Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Monday, 29 December 2025

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YAIPONGEZA NMB KWA UDHAMINI MNONO WA MAPINDUZI CUP

ZANZIBAR – Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza Benki ya NMB kwa kusaini mkataba mnono wa udhamini wa Mashindano ya Mapinduzi Cup, hatua iliyobadili rasmi jina la mashindano hayo na sasa kuitwa NMB Mapinduzi Cup.

Udhamini huo unaanza rasmi na mashindano ya NMB Mapinduzi Cup 2026, yatakayoshirikisha timu 10 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Uganda.

Timu Zitakazoshiriki NMB Mapinduzi Cup 2026

Mashindano hayo yatashirikisha:

  • Tanzania Bara: Yanga, Simba SC, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United
  • Zanzibar: Mlandege, KVZ, Fufuni FC na Muembe Makumbi City
  • Timu mwalikwa: URA FC ya Uganda

Michuano hiyo inatarajiwa kufikia tamati Januari 13, siku moja baada ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

SMZ Yasifu Uzalendo na Ushirikiano wa NMB

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Riziki Pembe Juma, aliishukuru Benki ya NMB kwa kuyapa hadhi na thamani mashindano hayo, akieleza kuwa udhamini huo ni kielelezo cha uzalendo na ushirikiano wa kweli kati ya sekta binafsi na Serikali.

Alisema mkataba huo ni muendelezo wa ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya NMB na SMZ, huku Serikali ikiahidi kuudumisha kwa manufaa ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla.

NMB mmetuonesha uzalendo mkubwa kwa kukubali kusaini mkataba huu kwa niaba ya Serikali. Udhamini huu si tu kubadili taswira ya mashindano, bali ni mkubwa na mnono zaidi kuwahi kutolewa,” alisema Waziri Pembe.

Aliongeza kuwa hata tuzo za Fair Play kwa wachezaji zitakazotolewa katika hatua mbalimbali za mashindano zinaonesha dhamira ya NMB ya kuyaimarisha na kuyaongezea mvuto mashindano hayo.

NMB: Udhamini Ni Kuitangaza Zanzibar na Tanzania Kimataifa

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema benki hiyo inajivunia ushirikiano wa zaidi ya miaka 13 na mashindano ya Mapinduzi Cup.

Alieleza kuwa udhamini huo ni sehemu ya juhudi za NMB kuunga mkono SMZ na kuitangaza Zanzibar na Tanzania kimataifa kupitia michezo.

Udhamini huu si kwa ajili ya NMB Mapinduzi Cup 2026 pekee, bali ni mchango wa NMB katika kuitangaza Zanzibar na Tanzania kimataifa, ambayo ndiyo dhana halisi ya ushiriki wa sekta binafsi,” alisema Donatus.

Alifafanua kuwa NMB itashirikiana na Kamati ya Maandalizi katika masuala ya uendeshaji wa mashindano, ikiwemo utoaji wa tuzo za Mchezaji Mwenye Nidhamu (Fair Play) katika kila mchezo.

Zawadi za Fair Play

  • Hatua ya makundi: Sh. 500,000
  • Nusu fainali: Sh. 1,000,000
  • Fainali: Sh. 2,000,000 (itakayotolewa mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi)

Kamati Yaipongeza NMB Kwa Kuipa Hadhi ya Kimataifa Michuano

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri Pembe, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya NMB Mapinduzi Cup 2026, Machano Makame Haji, aliishukuru NMB kwa kuyabeba mashindano hayo na kuyafanyia maboresho makubwa yanayoyawezesha kuwa na hadhi ya kimataifa.

Mbele ya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Ali Abdulghulam Hussein, alisema makubaliano kati ya Kamati na NMB yalifikiwa kwa haraka kutokana na dhamira njema ya pande zote.

Naye Katibu wa Mashindano hayo, Rashid Said Suleiman, alisema mkataba huo ni hatua muhimu katika ukuaji na maendeleo ya michezo, hususan mpira wa miguu Zanzibar.

Mkataba huu unaipa Kamati uhakika wa kifedha, jambo litakalosaidia kuimarisha ubora na ushindani wa mashindano,” alisisitiza.

 

No comments:

Post a Comment