ZANZIBAR — Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya jamii kwa kujivunia ushiriki na udhamini wake katika matukio mbalimbali yanayoambatana na Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ikiwemo Siku ya Kitaifa ya Mazoezi.
Hayo yamebainika baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuitunuku benki hiyo Cheti cha Shukrani na Pongezi kwa kufadhili, kudhamini na kushiriki kikamilifu katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi. Cheti hicho kilitolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kufuatia kukamilika kwa matembezi maalum yaliyoanzia Viwanja vya Mapinduzi Square Michezani hadi Uwanja wa New Amaan, ambapo mazoezi ya viungo ya pamoja yalifanyika.
Katika kufanikisha matembezi na mazoezi hayo yaliyoshirikisha zaidi ya watu 6,000 kutoka vikundi zaidi ya 170 vya mazoezi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, NMB ilikabidhi tracksuit 100 kwa viongozi waandamizi wa SMZ wakiongozwa na Rais Dk. Mwinyi pamoja na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.
Akihutubia washiriki wa mazoezi hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza wadhamini wote kwa mchango wao katika kufanikisha Siku ya Kitaifa ya Mazoezi, akisisitiza kuwa mchango huo una thamani kubwa kwa ustawi wa afya za Wazanzibar. Aliwahimiza wananchi kudumisha utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara.
“Nawashukuru wadau na wafadhili wote waliotoa michango yao katika kufanikisha bonanza hili linaloandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Mchezo wa Mazoezi Zanzibar (ZABESA). Mazoezi ya viungo ni muhimu kwa afya ya mwili na akili, na husaidia kukinga magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo,” alisema Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kuwakumbusha wananchi kuwa afya njema ni nyenzo ya msingi ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, huku akisisitiza ushiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha na michezo ya majini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Nassor, alisema benki hiyo inajivunia siyo tu ufadhili na ushiriki wake katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi, bali pia mchango wake wa jumla katika Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Nassor, ambaye pia ni Meneja wa NMB Tawi la Mwanakwerekwe, alisema kwa kipindi cha miaka 13, NMB imekuwa ikishiriki na kudhamini matukio mbalimbali yanayokuwa sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Mapinduzi, ikiwemo kudhamini mashindano ya soka ya NMB Mapinduzi Cup.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango wetu na kutupatia cheti cha shukrani kwa ufadhili wa bonanza hili. Kama benki, tunajivunia mchango wetu katika matukio yanayoambatana na sherehe hizi, ikiwemo kutoa tracksuit 100 kwa viongozi wa SMZ na kuwa wadhamini wakuu wa NMB Mapinduzi Cup,” alisema Nassor.
Alisisitiza kuwa NMB, kama benki inayojali afya na ustawi wa jamii, itaendelea kushirikiana na SMZ katika kuendeleza na kuhamasisha shamrashamra za Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yanayotimiza miaka 62 mwaka huu.
.jpeg)



No comments:
Post a Comment