Dar es Salaam, Tanzania – Katika zama za mabadiliko ya haraka ya kiuchumi, Equity Bank Tanzania imeonyesha dhamira thabiti ya kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa, huku ikiwekeza katika suluhisho za kifedha zinazolenga kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kwa kiwango cha juu.
Akizungumza katika uzinduzi wa bidhaa mbili mpya za Mastercard – Black Card na Yellow Card jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Bi. Isabela Maganga, alisema kuwa benki hiyo inalenga kujipanga kimkakati kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya uchumi unaokua kwa kasi.
“Takwimu zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi. Sisi kama taasisi ya kifedha, tunahitaji kwenda sambamba na hali hiyo kwa kuanzisha huduma zinazowezesha Watanzania kupata fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi,” alisema Bi. Maganga.
Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi na Kijamii
Bi. Maganga aliongeza kuwa kupitia huduma mpya za Mastercard, wateja wa Equity Bank watapata fursa ya kutumia huduma za kifedha popote walipo duniani, hatua inayolenga kuongeza uwezo wao wa kufanya biashara katika soko la kimataifa.
“Benki yetu inatambua umuhimu wa huduma za kifedha zilizo salama, rahisi na zinazokidhi mahitaji ya dunia ya leo. Mastercard Black Card na Yellow Card ni zaidi ya kadi – ni nyenzo za kuwawezesha wananchi kufikia malengo yao ya kifedha na kijamii,” alisisitiza.
Serikali Yapongeza Mwelekeo Mpya wa Kibenki
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, aliipongeza Equity Bank kwa kuunga mkono ajenda ya serikali ya ukuaji wa uchumi jumuishi, hususan kwa wanawake na vijana.
“Serikali inajivunia kuona taasisi kama Equity Bank zikichangia ajenda ya maendeleo kupitia uwekezaji katika teknolojia na usalama wa kifedha. Hii ni hatua muhimu katika kukuza matumizi salama ya fedha, uwazi, na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa,” alisema Mahundi.
Kuelekea Mfumo wa Kifedha wa Kisasa
Kupitia uzinduzi wa Mastercard Black Card na Yellow Card, Equity Bank Tanzania inajidhihirisha kama mdau wa mabadiliko katika sekta ya fedha. Bidhaa hizi mpya ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuhimiza matumizi ya teknolojia za kifedha (FinTech) katika kuboresha upatikanaji wa huduma na kuchochea ustawi wa uchumi wa taifa.

Equity Bank Tanzania inaendelea kujenga mazingira jumuishi ya kifedha yanayochochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja, biashara ndogo, za kati, na sekta binafsi kwa ujumla. Kwa kuwekeza kwenye suluhisho za kisasa kama Mastercard, benki hii inachukua nafasi muhimu katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na maendeleo barani Afrika.
No comments:
Post a Comment