Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 11 July 2017

TANZANIA YATEULIWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 37 WA SHIRIKA LA MAKAZI AFRIKA 2018

Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Kyando Mchechu ambaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa 36 wa Shelter Afrique akisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wajumbe wa nchi 44 za kiafrika ambao ni wanachama wa chombo hicho cha makazi. Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Kingdom, Victoria Falls, Zimbabwe Julai 6, 2017.
● Kunufaika na kuvutia watalii

● Ni mkutano unaovuta wawekezaji na wafanyabiashara

● Mkutano huo huhuzisha nchi wanachama 44 wa Afrika

Na Muungano Saguya, Victoria Falls, Zimbabwe


Tanzania imeteuliwa kwa kauli moja na wajumbe wa Mkutano wa 36 wa Makazi Afrika (Shelter Afrique) kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 37 ambao utafanyika mwezi Julai 2018 Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ambao una wanachama kutoka nchi 44 za Afrika walikutana katika Mji wa Kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe ili kujadili changamoto za hali ya makazi kwa watu wa nchi hizo ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo kwa kutumia uzoefu wa kila nchi mwanachama. Aidha, katika Mkutano huo ambapo Tanzania iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Kyando Mchechu, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi, iliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo wa 36.

Mambo mbalimbali yalijadiliwa na kukubalika ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto ya Rasilimali Fedha inayozikabili nchi nyingi wanachama wa Umoja huo na kushindwa kuwapatia wananchi wa Afrika makazi bora na nafuu. Katika kuondoa changamoto hiyo Mkutano huo umeazimia kuongeza Daraja C la wanachama wa umoja huo ambalo litahusisha mashirika, taasisi za kifedha na nchi za nje ya bara la Afrika ili kupata fedha au kuwa na ubia wa pamoja wa kusaidia kuwapatia wananchi wa nchi wanachama makazi bora na nafuu. Kadhalika, nchi hizo za kiafrika zimekubaliana kuhakikisha kila nchi inakamilisha michango yake inayodaiwa ili kuwezesha umoja huo kuendelea kusaidia mikopo kwa nchi wanachama ya kugharamia miradi ya ujenzi wa nyumba. Kundi A la Umoja huo huhusisha nchi 44 za Afrika na Kundi B huhusisha Benki ya Afrika (ADB).

Kuteuliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 37 kumechangiwa na Wajumbe wengi kufurahishwa na mabadiliko yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na Rais Dkt John Pombe Magufuli amekuwa gumzo kubwa kwa Wajumbe wa Mkutano huo wa Makazi kila wakizungumzia changamoto zinazolikabili Bara la Afrika.

Faida zitakazopatikana katika Mkutano huo kufanyika nchini Tanzania ni pamoja na kukuza utalii wa Tanzania kwa Wajumbe hao kuelezwa fursa za utalii na kujionea kazi mbalimbali za wajasiriamali hususan wa sekta ya nyumba ambao hualikwa katika Mkutano huo. Aidha, ni fursa kubwa kwa nchi kujitangaza kibiashara na kuvutia wawekezaji kutoka Bara la Afrika.

Tanzania ilijiunga na Shelter Afrique mwaka 2003 na Mkutano wa 32 wa Shelter - Afrique uliofanyika N’djamena, Chad mwaka 2013 ulipitisha Azimio Namba GM/2013/005 la kuongeza Hisa kwa kila nchi mwanachama kwa lengo la kukuza mtaji wa kampuni hiyo na kuiwezesha kuweka nguvu zaidi katika masuala ya uendelezaji nyumba barani Afrika.

Shirika la Nyumba la Taifa limenufaika na mtaji huo ambapo mwaka 2002 lilikopeshwa Dola za Kimarekani 1.5 milioni na kuzitumia kujenga nyumba 212 eneo la Boko Jijini Dar es Salaam na mwaka 2011 lilikopeshwa fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 14.5 milioni mkopo uliotakiwa kurejeshwa katika kipindi cha miaka 10 na mkopo huo ulitumika kujenga nyumba za gharama nafuu zipatazo 558 katika maeneo mbalimbali nchini. Pamoja na kuikopesha NHC, Shelter Afrique imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani 27,500,000/= katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba nchini Tanzania.

Mkutano huo wa 36 umefanyika katika Mji wa Kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe zamani ikiitwa Southern Rhodesia, ambapo wajumbe walipata pia fursa ya kutembezwa kwenye vivutio vya kitalii vilivyopo katika Mji huo unaopakana na nchi ya Zambia, zamani ikiitwa Nothern Rhodesia. 


Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Kyando Mchechu ambaye alichaguliwa kwa kauli moja na Wajumbe wa Mkutano wa 36 wa makazi Afrika kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kwanza wa Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Kingdom, Victoria Falls, Zimbabwe Julai 6, 2017 akipitia mada mbalimbali katika Mkutano huo.   
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Nehemia Kyando Mchechu akiwa na Mwenyekiti na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa 36 wa Shelter Afrique wakiongoza ajenda mbalimbali zilizowasilishwa katika Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Kingdom, Victoria Falls, Zimbabwe Julai 6, 2017.
Mkurugenzi wa Hazina na Uendelezaji Biashara wa NHC, Bw. David Shambwe akipitia na kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zinajadiliwa na Wajumbe kutoka nchi 44 za Afrika waliohudhuria Mkutano huo uliofanyika katika Mji wa Kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Sehemu ya Wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika wa Mkutano wa 36 wa Shelter Afrique wakifuatilia ajenda mbalimbali zilizowasilishwa katika Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Kingdom, Victoria Falls, Zimbabwe Julai 6, 2017.
Wajumbe wakifuatilia Mkutano wa 36 wa Shelter Afrique Mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe. 
Zimbabwe ni moja ya nchi za kiafrika ambayo inathamini na kuenzi tamaduni za kiafrika. Hapa ni moja ya vikundi vya kitamaduni ambavyo vilipamba burudani mbalimbali kwa Wajumbe wa Mkutano wa Makazi wa nchi za Kiafrika uliofanyika Victoria Falls nchini Zimbabwe.

No comments:

Post a Comment