Na Aron Msigwa – MAELEZO
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wawekezaji (Round Table Investment Forum) na Marais wa nchi 5 za ukanda wa Afrika Mashariki utakaofanyika jijini Dar es salaam kuanzia Machi 25 hadi 26 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya mkutano huo Mkuu wa wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa Marais hao Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watahudhuria mkutano huo wakiwa wameambatana na jumla ya wawekezaji 350.
Amesema Tanzania kwa mara nyingine imepata heshima ya kuandaa mkutano huo na kufafanua kuwa wawekezaji hao wamekwisha anza kuwasili jijini Dar es salaam kuanzia Machi 22, Machi huku marais nchi hizo wakitarajiwa kuwasili jijini humo kuanzia Machi 24, 2015.
Amesema wakiwa nchini Tanzania Marais hao watashiriki kwenye mkutano wa wawekezaji utakaofanyika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Mwalimu J.K. Nyerere kuanzia Machi 23 hadi 26, watatembelea bandari ya Dar es salaam ili kuona namna nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki zinavyoshirikiana katika masuala ya ushuru wa forodha na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Amebainisha kuwa kabla ya kuaondoka nchini Tanzania Machi 26, 2015 Marais hao pia watatembelea miundombinu ya reli inayotumika kusafirisha mizigo nchi za maziwa makuu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika usafirishaji wa bidhaa mbalimbali baina ya nchi zao.
No comments:
Post a Comment