JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
UAMUZI WA SERIKALI YA
KENYA KUZUIA MAGARI YA KITALII YALIYOSAJILIWA TANZANIA KUINGIA UWANJA WA NDEGE
WA KIMATAIFA WA JOMO KENYATTA KWA AJILI YA KUCHUKUA NA KUSHUSHA WATALII
Tarehe 22 Desemba, 2014, Serikali ya Jamhuri ya Kenya ilitoa amri ya kuzuia magari ya kitalii yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio vya utalii katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Baada ya uamuzi huu wa Serikali ya Kenya, Waziri wa Maliasii na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu alifanya majadiliano na Waziri wa masuala ya utalii wa Serikali ya Kenya siku ya tarehe 16, Januari, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa kadhia hii. Matokeo ya mkutano wa Mawaziri hawa yalikuwa ni kusitishwa kwa muda katazo lililotolewa na Serikali ya Kenya kwa makubaliano kuwa yafanyike mazungumzo baina ya pande hizi mbili ndani ya kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe 16 Januari, 2015 ili kurekebisha Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya utalii wa mwaka 1985 kati ya nchi zetu mbili.
Hivyo,
vikao vya wataalam vimefanyika Dar es Salaam na Arusha hadi wiki ya kwanza ya
mwezi huu wa pili kwa maandalizi ya kikao cha mwisho cha Mawaziri upande wa
Tanzania kabla ya kukutana na wenzetu wa Kenya. Pamoja na kushauriana na Waziri
mhusika wa Kenya (Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii, Bi. Phyllis
Kandie) kusogeza mbele tarehe ya mkutano wa pamoja ili kuruhusu muda wa kutosha
kwa majadiliano ya ndani na wadau, Bi. Kandie alimwandikia Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dkt. Richard Sezibera na kumnakili Waziri
Nyalandu, kurejesha amri yake ya awali ambayo alisema inaendana na Sheria ya
utalii na kanuni za uchukuzi za Kenya.
Serikali
ya Tanzania kimsingi imesikitishwa na uamuzi huo wa Serikali ya Kenya kwani
haujengi wala hauendani na dhamira njema ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya kuenzi njia ya mazungumzo, maelewano na maridhiano katika
kufikia maamuzi. Suala la kurekebisha mkataba ulioingiwa na nchi hizi mbili kwa
hiari miaka 30 iliyopita, si jepesi la kujadiliwa na Mawaziri wawili tu na
kuwekeana ukomo wa muda katika kulipitia. Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato
iliouanzisha wa kuhusisha wadau wote na kufikia uamuzi ambao itauwasilisha kwa
Serikali ya Kenya kupitia vikao rasmi vya Jumuiya.
Pamoja na
kwamba amri hii ya Serikali ya Kenya inaenda nje ya mkataba wa 1985 kwa
kuvihusisha hata viwanja vya ndege kuwa sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali
ya Tanzania itaheshimu na kuzingatia amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki
uliopo kati ya nchi zetu huku tukitafakari hatua za kuchukua ili kuondoa
bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wetu wanaopitia uwanja huo
wa Jomo Kenyatta. Aidha Tanzania itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na
wageni wote wenye nia ya kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia
viwanja vingine vya ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Kwa
upande wa Tanzania, viwanja vya ndege hasa vile vya Kimataifa vitaendelea kuwa
sehemu ya malango ya kuingilia na kutokea kwenda kokote iwe ndani ya Jumuiya au
nje ya Jumuiya na havitavichukuliwa kama vivutio vya utalii. Tanzania haitazuia
magari ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote
kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia
katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi zao.
Mkataba
wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa ushirikiano
katika Sekta ya Utalii kati ya nchi zetu mbili. Aidha, makubaliano hayo
yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya kubadilishana watalii huku ikizingatiwa
kuondoa bugudha kwa watalii. Maeneo hayo ni pamoja na miji ya mipakani pamoja
na miji rasmi iliyopendekezwa na kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi
ambako kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Mwisho,
Tanzania itaendelea kuenzi undugu na urafiki uliojengeka kwa zaidi ya miaka 50
tokea uhuru kati ya nchi zetu mbili na suala dogo kama hili halitaweza
kuteteresha uhusiano wetu mzuri.
WIZARA YA USHIRIKIANO
WA AFRIKA MASHARIKI,
10 FEBRUARI, 2015
No comments:
Post a Comment