Na Mwandishi Wetu, Pemba
Benki ya NMB imeonesha nguvu yake ya kifedha kwa kushiriki kwa kishindo katika Kongamano la Uwekezaji Zanzibar, lililoratibiwa na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kwa kutoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kushirikiana katika Mapinduzi ya Kiuchumi Visiwani humo.
Uimara wa NMB: Zaidi ya Bilioni 1.1 za Marekani
Mkuu wa Kitengo cha Miamala ya NMB, Bi. Linda Teggisa, aliwaeleza wawekezaji zaidi ya 1,000 waliokusanyika kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na mataifa mengine kuwa benki hiyo ina mtaji wa takribani USD 1.1 bilioni, na hivyo kuifanya kuwa benki kubwa zaidi Tanzania na ya pili kwa ukubwa Afrika Mashariki.
Aidha, NMB ni miongoni mwa taasisi chache za kifedha barani Afrika zilizoko kwenye “Klabu ya Kampuni Zenye Thamani ya Dola Bilioni Moja”, huku ikiwa imeweka rekodi ya faida baada ya kodi ya Shilingi Bilioni 643, pamoja na kulipa gawio la Shilingi Bilioni 214 kwa Serikali.
Mchango wa NMB Katika Uchumi wa Buluu
Bi. Linda alibainisha kuwa benki hiyo inaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar katika kukuza Uchumi wa Buluu, kwa kutoa huduma na masuluhisho maalum ya kifedha kwa wawekezaji wa viwango vyote.
“Asilimia 96 ya miamala ya NMB sasa inafanyika kidijitali, tukitumia teknolojia ya kisasa kutoa huduma kwa watu binafsi, kampuni kubwa na taasisi za serikali,” alieleza Linda.
Pia alisisitiza kuwa NMB ina uwezo mkubwa wa kusaidia kutekeleza Mipango Mkakati ya Serikali ya Zanzibar, hususan kuboresha maeneo ya uwekezaji kama Micheweni.
Wawekezaji wa Kimataifa Wavutiwa
Mwanzilishi wa Cocco Lagoon, Bw. Grzegorz Adamczak, alisema NMB ni benki iliyojipambanua hadi kufikia kuvutia wawekezaji wa kimataifa:
“Kwa rekodi na tuzo walizopata, NMB imejijengea heshima kubwa kimataifa na ni mshirika mzuri kwa wajasiriamali na wawekezaji wote.”