Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_211026

Stanbic Bank Banner_201026

Monday, 5 October 2026

VODACOM COASTAL CLASSIC YAUNGANISHA MICHEZO, UTALII NA MAENDELEO YA VIJANA AFRIKA

Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando (kushoto), akikabidhi tuzo kwa mshindi wa kwanza wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanawake, Mary Aleper (katikati) kutoka Uganda. Washindi wengine walikuwa Ditona Munu Martinie, mshindi wa pili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) (wa pili kushoto), na Mercy Elegae kutoka Kenya, aliyeshika nafasi ya tatu.
Washiriki wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic wakiwa katika eneo la kuanzia mbio hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Tehama wa Vodacom Tanzania PLC, Athumani Mlinga.

Bagamoyo, Pwani — 4 Oktoba 2026: Uzinduzi wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic umeonesha namna michezo inavyoweza kuwa chachu ya kukuza utalii, elimu na maendeleo ya jamii, huku mashindano hayo ya kuendesha baiskeli yakitoa fursa ya kuonesha vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda wa pwani ya Tanzania na kuunga mkono shughuli zenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii zinazopitiwa na msafara wa Nyerere Cycling Tour, zamani ukijulikana kama Twende Butiama.

Kwa kuwakutanisha waendesha baiskeli, jamii na wadau mbalimbali, mashindano hayo yamechangia kukuza utalii wa ndani, kuhamasisha vijana kupitia michezo na kusaidia jitihada za elimu na maendeleo katika maeneo yanayounganishwa na safari hiyo.

Washiriki wa Mashindano ya Nyerere Cycling Tour wakiendelea na safari katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kuelekea Bagamoyo.

Mashindano hayo, ambayo ni sehemu ya maandalizi kuelekea msafara wa Nyerere Cycling Tour, yaliwakutanisha waendesha baiskeli 147 walioshiriki mbio hizo zilizopita katika maeneo mbalimbali ya kuvutia ya ukanda wa pwani ya Tanzania.

Mbali na kutoa ushindani kwa waendesha baiskeli, mashindano hayo yameendelea kuonesha fursa za utalii nchini na kuongeza uelewa kuhusu shughuli za elimu, afya na uhifadhi wa mazingira zitakazotekelezwa katika maeneo mbalimbali wakati wa safari ya msafara huo kuelekea Butiama.

Afisa Mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Charles Maguzu, aliwapongeza waandaaji na washiriki wa mashindano hayo kwa kutumia michezo kama jukwaa la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ikiendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kituo cha utalii wa michezo.

“Vodacom Coastal Classic ni ushahidi wa namna mchezo wa baiskeli unavyozidi kuwa na nafasi muhimu katika kuhamasisha maisha yenye afya, kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji na kuonesha vivutio vya utalii vya Tanzania. Kupitia matukio kama haya, hatuendelezi vipaji vya michezo pekee, bali pia tunachangia katika elimu, uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii. Tunawapongeza Vodacom na washirika wote kwa kuendelea kuwekeza katika kukuza mchezo huu na kuhamasisha kizazi kijacho cha waendesha baiskeli,” alisema.

Kagimu na Aleper Washinda Vodacom Coastal Classic

Baada ya ushindani mkali, Charles Kagimu kutoka Uganda na Mary Aleper kutoka Uganda waliibuka washindi wa Vodacom Coastal Classic 2026 baada ya kumaliza katika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake, huku kila mmoja akizawadiwa shilingi milioni 10.

Mashindano hayo yaliwapa waendesha baiskeli fursa ya kutumia vipaji vyao kama chanzo cha kipato kupitia ushindani wa kitaaluma, huku yakihamasisha vijana zaidi kushiriki katika mchezo huo.

Washindi wa nafasi ya kwanza katika kila kundi walipata shilingi milioni 10, huku washindi wa nafasi ya pili wakipata shilingi milioni 7 na nafasi ya tatu shilingi milioni 5.

Waendesha baiskeli waliomaliza katika nafasi ya nne hadi ya kumi katika kila kundi walizawadiwa shilingi milioni 1 kila mmoja.

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando, aliwapongeza washindi pamoja na waendesha baiskeli wote walioshiriki, akieleza kuwa Vodacom Coastal Classic itaendelea kutoa fursa kwa waendesha baiskeli kuonesha vipaji vyao huku ikichangia katika malengo mapana ya maendeleo ya taifa.

“Zaidi ya ushindani wenyewe, Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour zinasaidia kukuza utalii wa ndani, kuunga mkono shughuli za elimu na kuhamasisha matokeo chanya ya kijamii katika jamii zinazopitiwa na safari hii. Tunajivunia kuwa sehemu ya jukwaa linalowawezesha vijana, wakiwemo wasichana, huku likitumia michezo kama nyenzo ya kuchochea maendeleo,” alisema.

Stanbic Bank Yaunga Mkono Mpango

Kwa upande wake, Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya benki hiyo katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

“Kwa miaka 30, Tanzania imekuwa zaidi ya soko kwa Stanbic Bank; ni nyumbani kwetu. Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour vinaonesha uwezo wa Tanzania katika utalii, vinawekeza katika elimu na vinafungua fursa kwa vijana na jamii kustawi. Kupitia ushirikiano huu tunawekeza kwa watu na jamii ambao maendeleo yao yataendelea kuijenga Tanzania ya kesho,” alisema.

Aliongeza kuwa Stanbic Bank itaendelea kuunga mkono mashindano hayo kupitia ushirikiano wake katika Nyerere Cycling Tour na jitihada za kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kushiriki mchezo wa baiskeli kama fursa ya michezo na uchumi.

Safari ya Nyerere Cycling Tour Kuelekea Butiama

Vodacom Coastal Classic ni sehemu ya shughuli zinazoambatana na Nyerere Cycling Tour, ambayo itahusisha safari ya kilomita 1,500 kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026.

Safari hiyo itawakutanisha waendesha baiskeli kutoka Tanzania na nchi nyingine, sambamba na shughuli zinazolenga kuhamasisha elimu, afya na uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali yatakayopitiwa.

Vodacom Tanzania PLC ndiye mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour, huku Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, BYD, ABC, Coca-Cola na Huawei zikiwa miongoni mwa washirika wanaounga mkono mpango huo kwa ujumla.

Kumalizika kwa mashindano ya Vodacom Coastal Classic sasa kunaweka msingi wa kuendelea kwa safari ya Nyerere Cycling Tour, huku waendesha baiskeli wakijiandaa kuendelea na safari kuelekea Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari zaidi kuhusu biashara, benki na fedha, pamoja na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini Tanzania.

Follow Kitomari Banking & Finance Blog

LinkedIn: https://www.linkedin.com/feed/
Facebook: https://www.facebook.com
Instagram: https://www.instagram.com
X (Twitter): https://x.com/home

Mshindi wa kwanza wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanaume, Charles Kagimu kutoka Uganda (katikati), mshindi wa pili Jordan Schleck kutoka Uganda (kushoto), na mshindi wa tatu Boniphace Ngwata kutoka Tanzania (kulia), wakionesha mfano wa hundi walizokabidhiwa katika mashindano hayo.
Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando (kulia), na mwanzilishi wa msafara wa baiskeli wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na washindi wa mashindano hayo upande wa wanawake. Mary Aleper kutoka Uganda, aliyeshika nafasi ya kwanza (katikati), Ditona Munu Martinie kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyeshika nafasi ya pili (wa pili kushoto), na Mercy Elegae kutoka Kenya, aliyeshika nafasi ya tatu (wa pili kulia).

No comments:

Post a Comment