Dodoma; Agosti 1, 2026 - Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Benki ya NMB kwa juhudi zake za kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi kupitia matumizi ya teknolojia na utekelezaji wa mkakati wa Rural Banking, akisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kukuza ujumuishi wa kifedha na maendeleo ya wananchi.
Akizungumza alipotembelea banda la NMB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kupunguza gharama za miamala ya kifedha ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma za kifedha kwa urahisi.
Akimkaribisha Waziri Mkuu katika banda hilo, Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo, alisema benki hiyo imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.
Alisema hadi sasa NMB imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.3 kwa sekta hizo, hatua inayochochea uzalishaji, kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Bi. Bishubo aliongeza kuwa benki hiyo imeendelea kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha, ikiwemo kuwawezesha vijana kupata mikopo ya hadi Shilingi milioni mbili kupitia mifumo ya kidijitali bila kuhitaji dhamana wala kufika katika tawi la benki.
Aidha, alisema huduma za Rural Banking zinaendelea kuwafikia wananchi moja kwa moja katika masoko, minada ya mifugo na maeneo mengine ya biashara vijijini, hatua inayosaidia kupunguza umbali wa kupata huduma za kifedha na kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo rasmi wa fedha.
Mbali na huduma za benki, NMB inaendelea kuwekeza katika utoaji wa elimu ya fedha kupitia programu ya NMB Kijiji Day, inayolenga kuwajengea wananchi uelewa wa masuala ya kifedha, usimamizi wa biashara na matumizi sahihi ya huduma za benki.
Pia benki hiyo imeendelea kushirikiana na vyuo vikuu nchini kuwaandaa vijana kwa kuwapa ujuzi unaohitajika katika uchumi unaozidi kutegemea teknolojia, ubunifu na maendeleo ya kidijitali.
Hatua hizo zinaendelea kuifanya NMB kuwa mmoja wa wadau wakuu katika kuendeleza ujumuishi wa kifedha nchini, huku ikiunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kupitia huduma za kifedha zinazowafikia wananchi wote, hususan waishio vijijini.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za uhakika, uchambuzi na taarifa za hivi karibuni kuhusu sekta ya benki, fedha na biashara nchini Tanzania.
.jpeg)
No comments:
Post a Comment