Dodoma | Agosti 9, 2026
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha wanawake, vijana na wakulima kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa suluhisho bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji halisi ya wakulima.
Hatua hiyo inafuatia Serikali kukabidhi Shilingi bilioni 300 kwa taasisi saba za kifedha, ikiwemo NBC, kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Akihitimisha Maadhimisho ya Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikabidhi mfano wa hundi ya Shilingi bilioni 300 kwa wakurugenzi wa taasisi hizo saba za kifedha.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuongeza fursa za kifedha kwa wanawake na vijana ili waweze kushiriki kikamilifu na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na sekta ya kilimo.
NBC YASEMA IPO TAYARI
Akizungumzia utayari wa NBC kutekeleza mpango huo, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa NBC, Bw. Jacob Nangi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini NBC katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya uwezeshaji.
Alisema benki hiyo imejipanga kuendelea kubuni bidhaa na suluhisho za kifedha zinazoendana na mahitaji ya vijana, wanawake na wakulima.
“Nisisitize utayari wetu wa kufanikisha mpango huu kulingana na malengo ya Serikali ya kuwasaidia vijana na wanawake nchini kushiriki na kunufaika kikamilifu na fursa mbalimbali zinazotokana na mnyororo mzima wa sekta ya kilimo,” alisema Bw. Nangi.
Alisema NBC imeenda hatua moja zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida za kibenki kwa wakulima, kwa kubuni suluhisho zinazolenga changamoto zinazojitokeza katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.
MALORI 28 KWA VYAMA VYA USHIRIKA
Katika kilele cha Maonesho ya Nanenane, NBC ilikabidhi rasmi malori 13 kwa Vyama Vikuu vya Ushirika vya RUNALI na Lindi Mwambao vya mkoani Lindi.
Kati ya malori hayo, 10 yamekwenda RUNALI na matatu Lindi Mwambao.
Makabidhiano hayo yamefanya idadi ya malori yaliyotolewa na NBC kwa vyama vya ushirika kufikia 28, baada ya benki hiyo kukabidhi malori mengine 15 kwa TANECU na KACU mapema wiki iliyopita.
Uwezeshaji huo unalenga kuongeza uwezo wa vyama vya ushirika kusafirisha mazao ya wakulima kwa ufanisi, kupunguza changamoto za usafirishaji na kuongeza thamani inayobaki kwa wakulima.
Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa, alisema mkopo wa malori 13 yaliyokabidhiwa RUNALI na Lindi Mwambao una thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.5.
“Unatarajiwa kuboresha ufanisi wa shughuli za ushirika na kuongeza uwezo wa wakulima kufikisha mazao yao kwenye masoko,” alisema Bw. Urassa.
WAKULIMA 57 WAPATA MIKOPO YA MAKAZI
Mbali na uwezeshaji wa usafirishaji wa mazao, NBC pia imeendelea kubuni bidhaa zinazolenga kuboresha maisha ya wakulima.
Katika kilele cha Nanenane, benki hiyo ilikabidhi mkopo wa uboreshaji wa makazi kwa Bw. Emmanuel Nyambi Masanja, mkulima na mwanachama wa AMCOS ya Kasandalala, iliyopo Ushetu wilayani Kahama.
Bw. Masanja ni miongoni mwa wakulima 57 ambao tayari wamewezeshwa na NBC kupitia mpango wa mikopo ya uboreshaji wa makazi kwa wakulima.
Bw. Nangi alisema hatua hizo zinaakisi mkakati wa NBC wa kwenda zaidi ya huduma za kawaida za kibenki kwa wakulima.
“Tunataka kutoa suluhisho zinazogusa mahitaji muhimu katika mnyororo mzima wa thamani—kuanzia uzalishaji, upatikanaji wa mitaji, usafirishaji na uhifadhi wa mazao hadi kuboresha maisha na makazi ya wakulima,” alisema.
MRAJIS: USHIRIKA NI DARASA KATI YA WAKULIMA NA BENKI
Hafla ya makabidhiano hayo ilishuhudiwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, ambaye alisema uwezeshaji huo unaendana na msisitizo wa Serikali wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za fedha na vyama vya ushirika.
Alisema ushirika una nafasi muhimu katika kuwaunganisha wakulima na taasisi rasmi za kifedha, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi na kupata huduma zinazokidhi mahitaji yao.
Dkt. Ndiege pia aliipongeza NBC kwa mpango wa mikopo ya uboreshaji wa makazi kwa wakulima, akisema unaweza kusaidia kubadilisha mtazamo wa muda mrefu wa kutoweka kipaumbele kwenye makazi bora kwa wakulima.
“Kupitia mpango huu wa mikopo ya uboreshaji wa makazi, wakulima wengi watashawishika kuingia kwenye ushirika ili wanufaike na fursa hii,” alisema.
Aliongeza kuwa mpango huo unawapa wakulima nafasi ya kuboresha makazi yao huku malipo yakifanyika baada ya kuuza mazao yao.
WAKULIMA: TUMEWEKWA KARIBU NA BENKI
Viongozi wa vyama vya ushirika vilivyonufaika na uwezeshaji huo pamoja na mkulima aliyepokea mkopo wa uboreshaji wa makazi waliipongeza NBC kwa kuendelea kubuni bidhaa zinazolenga mahitaji halisi ya wakulima.
Mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Bw. Ismail Nalinga, Mwenyekiti wa RUNALI, Bw. Odas Odas Mpunga, na mkulima Emmanuel Nyambi Masanja, walisema mfumo wa mauzo ya mazao kupitia vyama vya ushirika umeendelea kuimarika.
Bw. Mpunga alisema maboresho katika mfumo huo yameongeza uaminifu na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima.
“Mfumo wa mauzo ya mazao kupitia vyama hivi vya ushirika umeziwezesha benki kama NBC kuwa na msingi unaotuwezesha kunufaika na huduma zao, hususani mikopo, kwa usahihi zaidi. Kwa msingi huo, sisi kama wakulima kwa sasa tumekaribiwa na taasisi za fedha kuliko wakati mwingine wowote,” alisema.
Kwa ujumla, hatua za NBC zinaonyesha namna ushirikiano kati ya benki, vyama vya ushirika na Serikali unavyoweza kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wakulima—si katika kuongeza uzalishaji pekee, bali pia katika usafirishaji, upatikanaji wa masoko na kuboresha maisha ya familia za wakulima.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa muhimu kuhusu Benki, Fedha, Biashara na Uchumi Tanzania.
| Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa (wa pili kulia) akifafanua kuhusu huduma mbalimbali za benki hiyo mahususi kwa wakulima mbele ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege pamoja na wadau wengine. |
| Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa ufunguo wa gari Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Lindi Mwambao, Bw. Ismail Nalinga (wa pili), ikiwa ni ishara ya makabidhiano rasmi ya malori matatu (3) yaliyowezeshwa kupitia mkopo wenye riba nafuu kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Malori hayo yanalenga kuboresha usafirishaji wa mazao, kuongeza ufanisi wa shughuli za ushirika na kuimarisha kipato cha wakulima. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa (kulia) na Meneja wa Benki ya NBC tawi la Dodoma Bi Happyness Kizigira (kushoto). |
| Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa ufunguo wa gari Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha RUNALI, Bw. Odas Odas Mpunga (wa pili kulia), ikiwa ni ishara ya makabidhiano rasmi ya malori kumi (10) yaliyowezeshwa kupitia mkopo wenye riba nafuu kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Malori hayo yanalenga kuboresha usafirishaji wa mazao, kuongeza ufanisi wa shughuli za ushirika na kuimarisha kipato cha wakulima. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo wa NBC, Bw. Raymond Urassa (kulia) na Meneja wa Benki ya NBC tawi la Dodoma Bi Happyness Kizigira (kushoto). |
| Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Benki ya NBC, Bw. Jacob Nangi (katikati) akionyesha cheti cha kutambua ushiriki na udhamini wa benki hiyo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wengine wanaoonesha ishara ya ‘Tunakuona mbali’ ni maofisa waandamizi wa benki hiyo. |
| Tunakuona mbali mkulima! |
| Viongozi mbalimbali wa serikali waliapata wasaa wa kutembelea banda la NBC lilikuwepo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane 2026 yaliyohitimishwa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma mwishoni mwa wiki. |
No comments:
Post a Comment