Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Saturday, 20 June 2026

NMB YAONGEZA KASI YA KUFADHILI BIASHARA ZA MIFUGO, MIKOPO YAVUKA SH180 BILIONI

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, kuhusu mikopo, elimu ya fedha na huduma za kibenki kwa wafugaji alipotembelea banda la NMB katika Tri-Nations Livestock Expo 2026, Mbogo Ranches, Ubena Zomozi wilayani Chalinze, mkoani Pwani.

Ubena Zomozi, Chalinze; Juni 20, 2026 – Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini baada ya kutoa zaidi ya Sh180 bilioni kwa ajili ya kufadhili wafugaji na biashara mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mifugo.

Fedha hizo zimeelekezwa katika shughuli mbalimbali muhimu zikiwemo unenepeshaji wa mifugo, uzalishaji wa malisho, ununuzi wa mbegu bora za mifugo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa inayolenga kuongeza tija na ushindani katika sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Tri-Nations Livestock Expo 2026, yaliyofanyika katika viwanja vya Mbogo Ranches, Ubena Zomozi, Chalinze, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB Bank, Filbert Mponzi, alisema benki hiyo imeweka mkakati maalumu wa kuimarisha uwekezaji katika sekta ya mifugo kupitia huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wadau wa sekta hiyo.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, huku NMB ikiwa mdhamini mkuu wa tukio hilo kwa mwaka wa nne mfululizo.

Mponzi alisema NMB imeendelea kutoa mikopo kwa riba nafuu ya asilimia tisa, hatua inayolenga kuwapa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo fursa ya kupanua shughuli zao kwa gharama nafuu.

Alifafanua kuwa kupitia mikakati ya Agribusiness na Agri-Wholesale, benki hiyo inafadhili wafugaji, wazalishaji wa malisho, wanunuzi wa mifugo, wasindikaji wa mazao ya mifugo pamoja na biashara kubwa zinazohusiana na sekta hiyo.

Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya mifugo katika uchumi wa taifa na maisha ya wananchi. Ndiyo maana tunaendelea kubuni suluhisho za kifedha zinazowawezesha wadau wa sekta hii kuongeza uzalishaji na thamani ya biashara zao,” alisema Mponzi.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Dk. Nchemba aliwahimiza wafugaji kutumia elimu, ubunifu na teknolojia zinazopatikana kupitia maonesho hayo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, hususan uhaba wa malisho na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema matumizi ya mbinu za kisasa za ufugaji yatachangia kuongeza uzalishaji, kuboresha afya ya mifugo na kuinua kipato cha wafugaji nchini.

NMB imesisitiza kuwa itaendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wafugaji kupitia mtandao wake wa matawi 248, mawakala zaidi ya 75,000 pamoja na majukwaa ya kidijitali yanayowezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa urahisi.

Mbali na mikopo, benki hiyo inaendelea kutoa elimu ya fedha, ushauri wa biashara na huduma za bima kwa wafugaji, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuchochea ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo nchini.




No comments:

Post a Comment