Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Monday, 13 April 2026

WAKAZI WA DAR ES SALAAM WAIPONGEZA BENKI YA NMB KWA KUZINDUA MATAWI YANAYOTEMBEA (BANK ON WHEELS)

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio (wa nne kushoto), akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo, wakati wa uzinduzi rasmi wa utoaji huduma kupitia magari maalum (Matawi Yanayotembea), uliofanyika jijini Dar es Salaam. Magari hayo nane ni sehemu ya mkakati endelevu wa usambazaji Huduma za Kibenki Vijijini 'NMB Rural Banking Strategy'.
Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya Benki ya NMB, Donatus Richard (katikati), akimhudumia Mwajuma Athumani Saidi aliyehudhuria uzinduzi rasmi wa utoaji huduma kupitia magari maalum (Matawi Yanayotembea - Bank on Wheels), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam, Aprili 10, 2026: Katika hatua nyingine ya kuendeleza ujumuishaji wa kifedha nchini, NMB Bank Plc imezindua rasmi huduma za Matawi Yanayotembea—maarufu kama Bank on Wheels—ikiwa ni utekelezaji wa vitendo wa kaulimbiu yake ya Karibu Yako. Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam umepokelewa kwa shangwe na wakazi pamoja na wadau wa biashara, waliopongeza ubunifu huo unaolenga kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi.

Mapema mwaka huu, benki hiyo ilitambulisha magari maalum nane yatakayotoa huduma jumuishi za kibenki kwa wateja walioko mijini na vijijini. Matawi hayo yanayohama-hama yanalenga kufikia maeneo yenye shughuli nyingi za kiuchumi kama masoko, minada ya mifugo, machimbo ya madini na maeneo ya kilimo—ambapo mahitaji ya huduma za kifedha ni makubwa lakini upatikanaji wake umekuwa changamoto.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Alhamisi, Aprili 9, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi wa NMB, Donatus Richard, alisema kuwa huduma hiyo ni sehemu muhimu ya mkakati wa benki hiyo wa kusambaza huduma za kifedha vijijini kupitia NMB Rural Banking Strategy.

Alieleza kuwa magari hayo yatagawanywa katika kanda mbalimbali nchini, zikiwemo Dar es Salaam, Zanzibar, Kanda ya Kati, Kusini, Kaskazini, Ziwa, Magharibi na Nyanda za Juu Kusini, kwa lengo la kuwafikia zaidi ya wateja milioni 10 waliopo na kuvutia wengine kujiunga na benki hiyo.

Magari haya ni zaidi ya fursa kwa wateja wetu—hasa wajasiriamali na wafanyabiashara waliopo kwenye masoko na minada. Yatawapatia huduma za kifedha, ushauri, mikopo, bima pamoja na elimu ya fedha kwa ukaribu zaidi,” alisema Donatus.

Aliongeza kuwa tafiti zinaonesha taasisi nyingi za kifedha zimejikita zaidi mijini, hali inayosababisha pengo la huduma vijijini. NMB imechagua kubadili mwelekeo huo kwa kuwafuata wananchi walipo, ili kupunguza gharama na muda wa kupata huduma za kifedha.

Uzinduzi wa huduma hizi unakuja sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa mwaka 2026 hadi 2030 (MTP Agenda 2030), unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi yote ya jamii.

Kwa upande wa watumiaji, huduma hiyo imeonekana kuwa mkombozi mkubwa kwa wafanyabiashara na wananchi wa kawaida. Hellen Mushi, mfanyabiashara wa duka la simu katika Jengo la Manzese Plaza, alisema ubunifu huo unawapunguzia adha ya kupoteza muda kufuata huduma za kibenki matawini.

Hii Bank on Wheels imenivutia sana. Inatupa uhuru sisi wafanyabiashara kupata huduma haraka bila kusimamisha biashara zetu. NMB wanaendelea kuthibitisha kuwa wako karibu na wateja wao,” alisema Hellen.

Naye Elias Masangu Waburuba, mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga, alibainisha kuwa huduma hiyo itasaidia kupunguza hatari zinazotokana na matumizi ya fedha taslimu katika maeneo ya biashara kama minada na magulio.

Huduma hizi zitapunguza vihatarishi kama wizi na upotevu wa fedha. Ni suluhisho muhimu kwa wafanyabiashara wa vijijini na maeneo ya pembezoni,” alisema.

Kwa ujumla, wakazi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam—ikiwemo Manzese Darajani—wakiwemo madereva wa malori, mama lishe na wauza mitumba, wameipongeza NMB kwa kuendelea kuwa kinara wa ubunifu katika sekta ya fedha.

Kupitia huduma za kidijitali kama NMB Mkononi, mtandao mpana wa mawakala zaidi ya 73,000, na sasa Matawi Yanayotembea, NMB Bank Plc inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kujenga uchumi jumuishi na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kifedha kwa urahisi, usalama na kwa wakati.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio (kulia), akishuhudia mfanyakazi wa benki hiyo akimhudumia mmoja wa wateja ndani ya magari maalum ya kutoa huduma za kibenki (Matawi Yanayotembea - Bank on Wheels), aliyehudhuria uzinduzi rasmi wa utoaji huduma wa magari hayo.

No comments:

Post a Comment