Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Global Sanctions Compliance Masterclass

Tuesday, 3 March 2026

NBC ‘YAIPAMBA’ DABI YA KARIAKOO, YAANDAA FUTARI MAALUM KWA WADAU NA WATEJA

Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Binafsi (wadogo na wakubwa) wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bw. Elibariki Masuke (kulia), akikabidhi tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya NBC kwa Pedro Goncalves wa Young Africans Sports Club. Tukio hilo lilifanyika muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi ya Yanga dhidi ya Simba Sports Club maarufu kama ‘Kariakoo Derby’, iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Pambano hilo lilimalizika kwa sare tasa ya 0-0.
Mkuu wa Idara ya Sheria wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bw. Edward Lyimo (kulia), akimkabidhi tuzo kipa wa Young Africans Sports Club, Djigui Diarra, aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyowakutanisha Yanga dhidi ya Simba Sports Club maarufu kama ‘Kariakoo Derby’, iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Zanzibar, Machi 2, 2026 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Jumapili iliipamba mechi ya watani wa jadi Young Africans Sports Club (Yanga) na Simba Sports Club maarufu kama Kariakoo Derby, kwa kuandaa matukio maalum kwa wapenzi wa soka na wateja wake.

Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, na kuvuta hisia za maelfu ya mashabiki uwanjani pamoja na mamilioni ya watazamaji kupitia matangazo ya moja kwa moja.


Futari Maalum na Mtandao wa Urafiki

Kabla ya kuanza kwa pambano hilo, NBC iliandaa futari maalum kwa wateja wake na wadau wa soka. Tukio hilo lilitoa fursa ya kukutana, kubadilishana mawazo na kuimarisha mahusiano katika mazingira ya kirafiki na kimichezo.

Baada ya futari, wageni hao waliwezeshwa kusafiri kwa msafara maalum kuelekea uwanjani, ambako walishuhudia mechi hiyo kutoka jukwaa la VIP kwa hadhi ya kipekee. Licha ya pambano hilo kumalizika kwa sare tasa ya 0-0, presha na burudani ya dabi hiyo vilitosha kuwapa mashabiki thamani kamili ya muda wao.


Tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi

Shughuli hizo ziliongozwa na maofisa waandamizi wa NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Binafsi (wadogo na wakubwa), Bw. Elibariki Masuke. Katika hafla hiyo, tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya NBC ilikabidhiwa kwa kocha wa Yanga, Pedro Goncalves.

Tukio hilo lilishuhudiwa na mashabiki waliokuwa uwanjani pamoja na watazamaji waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni mbalimbali.


‘Screen’ Kubwa Mikoa Tofauti

Mbali na Zanzibar, NBC pia iliweka screen kubwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Moshi na Mbeya. Hatua hiyo ililenga kuhakikisha mashabiki wengi zaidi wanapata fursa ya kushuhudia dabi hiyo kubwa zaidi nchini na mojawapo ya mechi zenye mvuto mkubwa Afrika Mashariki.

Nje ya uwanja wa New Amaan Complex, maofisa wa NBC walitoa huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo utoaji wa tiketi za kielektroniki, kufungua akaunti na ushauri wa kifedha – wakionesha kwa vitendo kuwa udhamini wao unaenda sambamba na utoaji wa huduma bora.


NBC: Soka ni Uzoefu, Si Dakika 90 Pekee

Akizungumza wakati wa futari hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa NBC, Bw. Godwin Semunyu, alisema benki hiyo inaendeleza utamaduni wa kutumia mechi kubwa kama Kariakoo Derby kujenga na kuimarisha mahusiano na wateja pamoja na wadau wa soka.

Udhamini wetu hauishii tu kuboresha ligi tunazodhamini, bali pia kuhakikisha wadau wetu – wakiwemo wafanyakazi, uongozi na wateja – wanakuwa sehemu ya moja kwa moja ya mchezo huu. Tunataka soka liwe uzoefu, si tukio la dakika 90 pekee,” alisema.

Aliongeza kuwa NBC inaendelea kubuni mikakati mipya ya kuiboresha Ligi Kuu ya NBC kwa lengo la kukuza vipaji, kuongeza ushindani, kuchochea ajira kupitia michezo na kuimarisha hamasa ya soka nchini.


Mageuzi Chanya Kupitia Udhamini

Katika misimu ya hivi karibuni, imeonekana wazi kuwa udhamini wa NBC umeleta mageuzi makubwa katika soka la Tanzania. Mbali na kuziwezesha klabu kufanya usajili bora, benki hiyo imechangia utoaji wa huduma za kifedha kama bima ya afya na mikopo ya usafiri kwa timu, pamoja na kudhamini hafla za utoaji wa vikombe na tuzo mbalimbali.

Kwa mara nyingine tena, Kariakoo Derby imekuwa zaidi ya mechi — imekuwa jukwaa la kuunganisha wadau, mashabiki na taasisi za kifedha katika kusherehekea mchezo unaogusa mioyo ya Watanzania wengi.






No comments:

Post a Comment