Dar es Salaam — Katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini, Benki ya Stanbic Tanzania imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 19.9 kwa Taasisi ya Moyo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa rasmi na Meneja wa Benki ya Stanbic Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Edditrice Marco, kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Muhimbili, Dkt. Tatizo Waane. Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Bi. Edditrice alisema msaada huo umetolewa kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii wa Benki (Corporate Social Investment – CSI), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu benki hiyo kuanza kutoa huduma zake nchini Tanzania.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu, tunalenga kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuwawezesha watoa huduma za afya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Hii ni moja ya njia ambazo Benki ya Stanbic inazitumia kusherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania,” alisema Bi. Edditrice.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Muhimbili, Dkt. Tatizo Waane, aliishukuru Benki ya Stanbic kwa msaada huo, akieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma za matibabu ya moyo na kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa.
Aidha, Dkt. Waane alitoa wito kwa taasisi na mashirika binafsi kuendelea kushirikiana na sekta ya afya kupitia michango na ushirikiano wa kijamii, ili kuboresha zaidi huduma za afya nchini na kusaidia kupunguza mzigo wa magonjwa kwa wananchi.
Hatua ya Benki ya Stanbic inaendelea kuonesha dhamira ya taasisi binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, hususan katika sekta nyeti ya afya, sambamba na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment