Dar es Salaam, Oktoba 20, 2025 – Taasisi isiyo ya kiserikali ya Bluu imeendeleza kampeni yake ya “JAMBO KUBWA LINAKUJA, BLUU INATAWALA” kwa kutoa msaada wa kifedha kwa wanawake wajasiriamali katika masoko ya Makumbusho na Kawe, hatua inayolenga kuwawezesha kukuza mitaji na kuboresha biashara zao.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa tukio hilo, Mwakilishi wa Bluu, Bw. Hamisi Athumani, maarufu kama Mr. Bluu, alisema msaada huo ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo wa kuwawezesha kiuchumi makundi maalumu nchini, hususan wanawake wajasiriamali wadogo.
“Lengo letu ni kuwawezesha kiuchumi wanawake wajasiriamali wadogo ili waweze kufanikisha malengo yao na kupiga hatua katika maisha yao ya kiuchumi,” alisema Bw. Athumani.
Aliongeza kuwa msaada huo ni hatua ya awali tu katika safari ya Bluu ya kufikia wananchi wengi zaidi nchini kote.
“Huu ni mwanzo tu. JAMBO KUBWA LINAKUJA, BLUU INATAWALA. Tunaendelea kuwasaidia makundi mbalimbali, na si kwa kiwango kidogo — tumejipanga kufanya zaidi,” alisisitiza.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake waliopokea msaada huo walieleza furaha na shukrani zao kwa taasisi ya Bluu, wakisema kuwa msaada huo umekuja kwa wakati muafaka na utasaidia kuimarisha biashara zao.
Bi. Lucy Mshambo, mmoja wa walionufaika, alisema:
“Tunashukuru sana kwa msaada huu. Umekuja wakati muafaka na utatupa nguvu mpya ya kuendeleza biashara zetu.”
Naye Bi. Zainabu Saidi aliongeza kuwa msaada huo utawasaidia kuongeza mitaji, kuongeza bidhaa na kuwavutia wateja zaidi.
Kampeni ya JAMBO KUBWA LINAKUJA, BLUU INATAWALA ni sehemu ya juhudi endelevu za Bluu katika kukuza uchumi wa wananchi kupitia uwezeshaji wa kifedha, hasa kwa makundi yanayohitaji msaada wa mtaji wa kuanzia au wa upanuzi wa biashara.

.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment