Kimanzichana, Mkuranga – Pwani, 15 Oktoba 2025:
Programu endelevu ya usambazaji wa elimu ya fedha, huduma jumuishi za kibenki, utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi vijijini, ‘NMB Kijiji Day’, imeendelea wikiendi iliyopita katika Kata ya Kimanzichana, wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Kampeni hii inayoendeshwa na Benki ya NMB kwa ushirikiano na Kampuni ya Taifa Gas, inalenga kufikisha elimu ya fedha na huduma jumuishi za kibenki kwa wananchi wa vijiji zaidi ya 2,000 visivyofikiwa na huduma rasmi za kifedha, sambamba na upandaji miti na bonanza la michezo mbalimbali.
Elimu ya Fedha kwa Vikundi vya Kijamii
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo, Meneja wa Kanda, Mauzo ya Vikundi na Huduma za Kibenki Vijijini wa NMB Makao Makuu, Dismas Prosper, aliwataka vikundi vya kijamii, wajasiriamali wadogo, mama lishe na waendesha bodaboda kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia NMB Kikundi Akaunti.
Alisisitiza umuhimu wa kuvirasimisha vikundi kwa kufungua akaunti hizo ili kunufaika na huduma za bima, mikopo, na huduma jumuishi za kifedha kidigitali, zinazosaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.
“NMB Kikundi Akaunti ni suluhisho la uhifadhi wa fedha za vikundi. Inawawezesha wanachama kujua namna ya kunufaika na pesa zao na kufikia malengo yao ya kifedha kwa urahisi zaidi,” alisema Prosper.
Aliongeza kuwa faida za akaunti hiyo ni pamoja na usalama wa fedha, urahisi wa kuweka akiba kidigitali, pamoja na taarifa sahihi za kifedha kwa kila mwanachama.
Aidha, aliwahamasisha wanachama wa vikundi kufungua akaunti binafsi ili kunufaika na huduma kama Mshiko Fasta, mkopo usiohitaji dhamana unaofikia hadi Shilingi Milioni 1.
Nishati Safi ya Kupikia kwa Maendeleo Endelevu
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Idara ya Mauzo wa Kampuni ya Taifa Gas, Henry Muya, alisema kampuni yake imejipanga kuhakikisha elimu ya utunzaji mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wote nchini.
Alisisitiza kuwa matumizi ya gesi si ya wakazi wa mijini pekee, bali ni kwa Watanzania wote, ili kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
“Ni muhimu kwa wananchi vijijini kuanza kutumia nishati safi ya kupikia. Hii itasaidia kupunguza ukataji miti na kulinda afya ya familia,” alisema Muya.
Ushuhuda wa Wananchi
Mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Abdallah Omar, alisema amevutiwa na elimu waliyoipata kuhusu NMB Kikundi Akaunti na bima za vikundi.
“Kupitia semina hii, tumejifunza namna ya kutunza fedha zetu kwa njia salama na za kisasa. Pia tumeona faida ya kurasimisha vikundi vyetu na kuwa na bima inayotusaidia hata tunapopatwa na majanga,” alisema.
Naye Mariam Suleiman, mwanachama wa Kikundi cha Wanawake na Maendeleo Kimanzichana, alisema elimu kuhusu bima ya afya ya vikundi imemgusa zaidi kutokana na changamoto za kumudu gharama za matibabu vijijini.
NMB Yaendelea Kujenga Uelewa wa Kifedha Nchini
Katika semina hiyo, washiriki walipata pia elimu kuhusu mikopo nafuu, bima, na matumizi sahihi ya fedha, yaliyotolewa na Meneja Mauzo - Benki Vijijini wa NMB Makao Makuu, Robert Mtimba, ambaye aliwasisitiza wananchi kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuboresha maisha yao kiuchumi.
Kupitia NMB Kijiji Day, Benki ya NMB inaendelea kujenga uelewa wa kifedha, kuongeza ushirikishwaji wa huduma za kibenki, na kuimarisha ustawi wa jamii vijijini kote nchini.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment