Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Tuesday, 17 December 2024
MRADI WA KUPAMBANA NA MALARIA WA $43 MILIONI WALETA MAFANIKIO NCHINI
Dar es Salaam – 12 Disemba 2024: USAID ilitangaza hitimisho ya miaka minne ya Mradi wa Udhibiti wa Vimelea vinavyosababisha Ugonjwa wa Malaria kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) uliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio katika mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi huu, zaidi ya vyandarua milioni 20 vyenye dawa ya kuua mbu waenezao ugonjwa wa malaria vimesambazwa katika Tanzania Bara na Zanzibar, vikiwalinda zaidi ya watu milioni 35. PMI kupitia USAID ilitoa vyandarua hivyo kupitia kampeni za umma katika shule za msingi na vituo vya afya, kwa kuzingatia makundi yaliyo hatarini zaidi ikiwa ni pamoja na watoto wachanga na wanawake wajawazito.
"Ushirikiano wa Marekani na Tanzania umedumu kwa zaidi ya miongo sita, na tangu mwaka 2006, PMI imewekeza zaidi ya dola milioni 747 kupambana na malaria nchini Tanzania," alisema Craig Hart, Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania. "Tunajivunia mafanikio ya Mradi wa Udhibiti wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa malaria wa PMI. Ingawa mradi huu maalum umemalizika, dhamira yetu ya kushirikiana na watu wa Tanzania na kushughulikia malaria na changamoto nyingine za afya ya umma bado haijabadilika."
Kati ya mwaka 2020 na 2024, mradi huu wa dola milioni 43, ukiongozwa na Kituo cha Programu za Mawasiliano cha Johns Hopkins kwa kushirikiana na Tropical Health LLP na Viamo PBC, uliunga mkono juhudi za kulinda asilimia 90 ya watu walioko hatarini. Hii ilijumuisha mikoa 14 yenye maambukizi ya juu ya malaria, Tanzania Bara na mikoa yote mitano ya Zanzibar, ikiwa ni jumla ya asilimia 57 ya idadi ya watu nchini Tanzania.
Mafanikio muhimu yalijumuisha kuimarisha uwezo wa mashirika ya usambazaji wa vifaa vya matibabu ya Tanzania kusimamia usambazaji wa vyandarua kwa uhuru, kuboresha vifaa vya usafirishaji kupitia zana za kisasa na mifumo ya kufuatilia kwa wakati halisi, na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa juhudi za kuzuia malaria.
Mshauri wa Mpango wa PMI nchini Tanzania, Naomi Serbantez, alisisitiza mafanikio ya mradi huu katika kuboresha upatikanaji wa vyandarua kwenye kaya na kuendeleza mikakati ya kudhibiti malaria inayotegemea ushahidi. Kwa kukuza utaalamu wa ndani na kutumia maarifa yanayotokana na takwimu, mradi huu umeweka msingi wa maendeleo endelevu katika kutokomeza malaria kote Tanzania bara na Zanzibar.
Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa hii, tafadhali wasiliana na Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani kupitia barua pepe: DPO@state.gov
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment