Dar es Salaam 29 Juni, 2021 – Benki ya CRDB imetangaza zawadi za washindi wa msimu wa pili wa CRDB Bank Marathon 2021 ambapo jumla ya shilingi milioni 45.4 zitatolewa kwa washindi 32. Akitangaza zawadi hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema kwa mwaka huu zawadi zimeongezwa ili kuendana na hadhi ya kimataifa ambayo CRDB Bank Marathon ilipewa mwaka huu baada ya kusajiliwa na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AMIS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).
“Mwaka huu sio marathon tu ni ya kimataifa, hata zawadi pia ni za kimataifa zaidi. Tumejipanga kutoa zawadi nono kwa washindi, kwa mbio kubwa za kilometa 42 mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 5, mshindi wa pili shilingi milioni 3, mshindi wa tatu shilingi mili 2 na mshindi wa nne shilingi milioni 1. Hizi ni zawadi kubwa zaidi kupata kutokea katika mbio zote nchini,” alisema Tully huku akibainisha kuwa wingi wa zawadi unatokana na kuongezeka kwa namba ya washiriki ambapo ambapo matarajio ni kupata washiriki 5,000 kutoka ndani nan je ya nchi.
Akizungumzia fursa zitokanazo na mbio hizo ambazo sasa hivi zimesajiliwa kimataifa, Tully alisema mbio hizo zitakwenda kuchochea uchumi wa Jiji la Dar es Salaam na kulitangaza jiji hilo pamoja na Tanzania kwa ujumla duniani kote. Alisema mbio hizo zitatumika kutangaza vivutio na historia ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo utamaduni wa pwani (swahili culture). “ Pamoja na hivyo mbio hizi pia zitasaidia kuonyesha vipaji vya wakimbiaji duniani kwani mbio hizi zitaonyeshwa live na TVE ambayo ipo DSTV. Tunakwenda kufunguka zaidi kwenye anga za dunia,” alisisitiza Tully.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikikisho Riadha Tanzania, Jackson Ndaweka aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo kwa viwango vya kimataifa huku akimhakikishia Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa kuwa zawadi zote zitabaki nchini kwani wanariadha sasa hivi wanajifua kuelekea tarehe 15 Agosti 2021 siku ya marathon. “Wanariadha wetu wana kiu kubwa ya kushindana baada ya mbio nyingi za kimataifa kuahirishwa kutokana na changamoto ya COVID-19. Zawadi hizi zimekuja wakati muafaka na wanariadha wetu wapo wanajifua kuchuana na wanariadha wa kimataifa,” alisema Ndaweka.
Kujisali na kuchangia katika CRDB Bank Marathon washiriki wanatakiwa kutembelea katika tovuti rasmi yam bio hizo www.crdbbankmarathon.co.tz ambapo mtu binafsi anatakiwa kuchangia shilingi 30,000 na washiriki kupitia vikundi ni shilingi 25,000. Malipo yanaweza kufanyika kupitia matawi ya Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App, mitandao ya simu na kupitia kadi ambazo zinawawezesha hadi watu wa nje ya nchi kufanya malipo.
No comments:
Post a Comment