Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 25 February 2020

BENKI YA CRDB YAPONGEZWA KUISAIDIA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR UKUSANYAJI WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 25 SEKTA YA UTALII


Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid akiwasili katika Semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyoandaliwa na Benki ya CRDB. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alipokuwa akimpokea.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Semina hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akiwasilisha mada wakati wa Semina na Baraza la Wawakilishi iliyoandaliwa na Benki hiyo wikiendi hii. Semina hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Idd akimpongeza Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kwa utayari wa Benki hiyo kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miradi ya maendeleo wakati wa Semina Maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Hoteli ya Verde, Zanzibar Wikiendi hii.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid akifuatilia mada katika Semina hiyo. Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akielezea ushiriki wa Benki hiyo katika kusaidia jamii Zanzibar kupitia miradi ya CSR.
Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts akifafanua jambo wakati wa Semina hiyo.
Wageni waalikwa wakifuatilia kwa makini mada katika semina hiyo.
Wageni waalikwa wakifuatilia mada katika semina hiyo.
Wageni waalikwa wakifualtiia kwa makini mada.
Waziri wa Afya SMZ, Hamad Rashid akichangia kuhusu uwekezaji katika huduma za afya kwa kujenga hospitali za kisasa ambapo alisema ni chachu katika kuimarisha nguvu kazi ya taifa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara SMZ, Mhe. Hassan Hafidh Khamis akichangia mada wakati wa Semina hiyo huku akiitaka Benki ya CRDB kuwekeza zaidi katika viwanda kwani vitasaidia kuongeza ajira hususan kwa vijana. 
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Tauhida Gallos akitoa mchango wake kuhusu uwezeshaji wa wakinamama wajasiriamali wakati wa Semina hiyo. 
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kwa jailli ya Bonanza kati ya Benki hiyo na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi lililofanyika wikiendi hii.


Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa kinara katika kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukusanya mapato katika sekta ya Utalii. Mwaka jana Benki ya CRDB kupitia mifumo yake ya kidijitali iliweza kukusanya kodi na tozo kwa watalii na wageni zinazofikia dola za kimarekani milioni 12 kutoka dola laki 4 mwaka 2014 ambapo ni ongezeko la takribani asilimia 3000.

Akizungumza katika Semina maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine wa taasisi za Serikali Mheshimiwa Zuberi Ali Maulid, alisema Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu katika uchumi wa Zanzibar hususani katika kuweka miundo mbinu thabiti ya huduma za kifedha kwa Wazanzibari na wageni.

“Benki ya CRDB ni mshirika muhimu katika uchumi wa Zanzibar, hususan kipindi hiki tukiwa tunakwenda kukamilisha Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020. Serikali inafurahishwa sana na namna ambavyo tumekuwa tukishirikiana na Benki hii katika kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Mhe. Zubeir Maulid.

Mheshimiwa Zubeir Maulid alisema moja ya mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata kutokana na ushirikiano baina yake na Benki ya CRDB ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambao unatokana na uunganishwaji wa mifumo ya kidijitali ya malipo ya Benki ya CRDB. “Mwaka jana wametusaidia kukusanya zaidi ya dola za kimarekani milioni 12, hiki ni kiwango kikubwa sana ambacho kinatokana na ufanisi wa mifumo hii ya kidijitali ya Benki ya CRDB,” alisema Mhe. Zubeir Maulid.

Mhe. Zubeir Maulid alisema kuongezeka kwa ukusanyaji huo katika sekta ya utalii kunasaidia kuongeza kwa Pato la Taifa, na hivyo kuiongeza serikali uwezo katika utoaji wa huduma za kijamii. Pia alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafurahishwa na ushiriki wa Benki ya CRDB katika sekta nyengine za maendeleo ikiwamo kilimo, biashara na viwanda pamoja na ujenzi wa miundombinu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema kwamba Benki ya CRDB imedhamiria kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia malengo ya kujenga nchi yenye uchumi wa kati kupitia uwezeshaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo. "Tunafahamu Serikali imejipanga kuleta mapinduzi katika sekta zote za maendeleo na sisi tumeweka mikakati ya ushiriki wetu katika kuisaidia Serikali kuanzia sekta ya kilimo, utalii, ujenzi, uchakataji wa mazao na uwekezaji kwenye viwanda,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa benki hiyo pia imejipanga pia kuwezesha sekta binafsi ambayo ni mshirika wa maendeleo wa Serikali nchini.

Nsekela alisema usahili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Tabianchi (GCF) ulioipata Benki hiyo mwishoni mwa mwaka jana umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo ambapo sasa hivi inaweza kutoa hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.

“Hizi ni fedha nyingi sana ambazo tumedhamiria kuzielekeza katika miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na Serikali na sekta binafsi,” aliongezea Nsekela.

Semina hiyo maalum kwa ajili ya Wajumbe na Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa Serikali Zanzibar ambayo ilikuwa na kauli mbiu ya “Pamoja Kujenga Uchumi”, ililenga katika kujadiliana namna ya kuboresha ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya CRDB katika kufanikisha miradi ya maendeleo nchini pamoja na kusogeza huduma za kibenki karibu zaidi na wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

No comments:

Post a Comment