Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday 17 October 2019

BENKI YA NMB YAZINDUA HUDUMA MPYA YA KUWANUFAISHA BODABODA

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, akiwa amepanda pikipiki wakati wa uzinduzi wa huduma ya Master Boda ambayo ni maalum kwa madereva wa bodaboda kujiwekea akiba jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama Barabarani, Abel Swai na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna.
Dar es Salaam, 16/10/2019: Benki ya NMB imezindua malipo ya kimtandao kwa huduma za bodaboda.

Mfumo huo wa malipo ni wa aina yake na wa kwanza nchini unaowawezesha abiria na wateja wa bodaboda kulipa nauli zao kwa kutumia simu zao za mkononi na fedha hizo kwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya NMB ya dereva husika.

Huduma hii iliyozinduliwa ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia huduma za benki sambamba na kuhamasisha utunzaji fedha kwa njia salama na za uhakika.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema huduma hii inaweka msingi wa kurasimisha sekta ndogo ya usafiri wa bodaboda.

"Mnachokifanya leo kina baraka zote za Serikali. Hiki kitawasaidia vijana kuongeza umakini kwenye shughuli zao na kuchangia uchumi wa Taifa," amesema Mhagama.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema huduma hiyo inatoa fursa kwa maelfu ya madereva wa bodaboda nchini kutumia huduma za benki hatua ambayo itaimarisha usalama wa fedha zao pamoja na wao wenyewe.

“Hii ni namna bora zaidi ya kurudisha uwajibikaji kwa shughuli za madereva wa bodaboda ambao mchango wao kwenye uchumi wa Taifa unatambulika. Tunazindua huduma hii jijini Dar es Salaam kisha tutaenda Mwanza, Arusha, Ruvuma, Dodoma na Mbeya wiki chache zijazo,” amesema Zaipuna.

Mfumo huo wa malipo utawasaidia madereva bodaboda kukuza biashara zao kwa kuwapunguzia adha ya kuhifadhi fedha taslimu na kuwapa fursa ya kuepuka matumizi yasiyokuwa na mpangilio.

“Kwa kutumia MasterCard QR, tunatoa huduma ya uhakika wa malipo kwa madereva bodaboda kutoka kwa watoa huduma wote na benki za biashara wanaotumia huduma hii. Malipo yatafanywa kwa kutumia simu ya mkononi yenye programu ya MasterCard QR na kupunguza hatari za kumiliki fedha taslimu. Huduma hii kwa bodaboda ni sehemu ya mkakati wa benki kufikisha huduma zake kwa watu wengi zaidi,” amesema Zaipuna .

Mwakilishi wa MasterCard Tanzania – Frank Molla amesema mfumo huo wa malipo ya kidijiti unakusudia kuwapa uhuru dereva na abiria wake wakati wote wa safari huku ukimuepushia dereva uwezekano wa kuporwa au kupoteza fedha zake.

“MasterCard inakusudia kuhamasisha na kuwezesha malipo ya kidijitali hapa nchini. Benki ya NMB inayo dira inayofanana nasi katika ujenzi wa miundombinu itakayoiwezesha jamii kufurahia ulimwengu wa malipo ya kimtandao kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” amesema.

Tayari Benki ya NMB imewajengea uwezo zaidi ya madereva 1,000 wa jinsi ya kutumia QR kufanikisha malipo kwa kutumia simu za mkononi. Mfumo huo unatarajiwa kuongeza usalama wa malipo ya kimtandao kwa sekta hiyo ndogo ya watoa huduma.

Kumlipa bodaboda, abiria anatakiwa kwenda kwenye simu yako – NMB Mkononi, piga *150*66# kupata menu na kuchagua kufanya malipo halafu ‘Scan to Pay.’ Pia ukiwa na simu janja nenda kwenye programu (App) ya NMB Mkonini ambako atachagua ‘Scan to Pay’ na kuendelea na maelekezo

Kuhusu NMB

NMB Bank Plc (NMB) ni benki ya biashara iliyosajiliwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa huduma za kibenki na fedha. Katika idara zake nne; wateja wadogo, wateja wakubwa, kilimo biashara na Hazina, NMB inatoa huduma zenye kiwango kinachokidhi mahitaji ya wateja wanaojumuisha wakulima, taasisi, kampuni na Serikali.

Benki ina matawi 220, zaidi ya mawakala 6,000 na zaidi ya mashine 800 za kutolea fedha (ATM) zilizopo nchini kote. Ina matawi katika wilaya zote za Tanzania. NMB ina zaidi ya wateja milioni tatu inaowahudumia na imeajiri zaidi ya wafanyakazi 3,000. Benki imeorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam na wanahisa wake wa kimkakati ni Rabobank mwenye asilimia 34.9 na Serikali ya Tanzania yenye asilimia 31.9 ya hisa zote.

Kwa miaka saba mfululizo (2013 hadi 2018), taasisi ya Euromoney imeichagua NMB kuwa ‘benki bora zaidi Tanzania.’ Jarida la Banker East Africa limeitunuku NMB tuzo ya benki bora Afrika inayoshirikiana na taasisi ya International Finance Cooperation (IFC) ya Benki ya Dunia na benki bora ya rejareja nchini Tanzania.

Kwa taarifa zaidi kuhusu NMB na huduma zake, tafadhali tembelea tovuti yetu: www.nmbbank.co.tz.

Kwa maswali au habari zaidi, tafadhali wasiliana na:
Rahma Mwapachu, 

Kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano,
Benki ya NMB,
Baruapepe: Rahma.Mwapachu@nmbtz.com

No comments:

Post a Comment