Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 26 September 2017

BENKI YA CRDB YATOA MSAADA WA SHILINGI MILIONI 100 KWA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KWA AJILI YA UJENZI WA OFISI ZA WALIMU SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI JIJINI DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kulia), akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni mia moja kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi za walimu kwa shule za msingi na sekondari Mkoa wa Dar es Salaam. Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi za mkuu wa Mkoa jana. Wengine kushoto ni Mkurugenzi wa Masoko Utafiti na Huduma kwa wateja wa Benki hiyo Tully Esther Mwambapa na Mwenyekiti wa Ujenzi wa ofisi hizo Kanali Charles Mbuge.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (katikati), akizungumza na waandishi wa habari katika hafla yakupokea msaada wa shilingi milioni mia moja za kitanzania kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi za walimu kwa shule za msingi na sekondari Mkoa wa Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei na kulia ni Mwenyekiti wa Ujenzi wa ofisi hizo Kanali Charles Mbuge.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei, (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari alipokwenda kukabidhi msaada wa shilingi milioni mia moja za kitanzania kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Dar es Salaam Tanzania, Septemba 25, 2017 Benki ya CRDB leo imekabidhi msaada wa shilingi milioni 100 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi za walimu kwa shule za msingi na sekondari mkoani humo. Msaada huo ni muendelezo wa utekelezaji wa sera ya kusaidia jamii ya Benki ya CRDB inayoelekeza kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka ili zitumike katika shughuli za kijamii kwenye maeneo ya afya, elimu na mazingira.

Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei alisema Benki hiyo inatambua kuwa elimu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa letu japo kuna changamoto nyingi zinazoikabili. “Tunatambua kuwa ili taifa letu liweze kupiga hatua za kimaendeleo, ni lazima tuungane kwa pamoja na kuwekeza katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ufundishwaji, jambo ambalo litaboresha viwango vya elimu yetu na kuleta matokeo chanya”  alisema Dokta Kimei.

Dokta Kimei alisema Benki ya CRDB imekuwa ikitoa misaada mbalimbali katika sekta ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maktaba, matundu ya vyoo, vitabu pamoja na vifaa mbalimbali vya kufundishia ambapo mwaka jana (2016) Benki hiyo ilichangia kiasi cha shilingi milioni mia moja kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa madawati mkoani Dar es Salaam.

 “Tunajivunia kuwa wadau wakubwa wa maendeleo ya elimu nchini ambapo kwa mwaka huu 2017 pekee, tayari Benki ya CRDB imeshatumia zaidi ya shilingi milioni mia tatu katika kufadhili ujenzi wa majengo ya madarasa katika shule mbalimbali nchini, ikiwamo shule za msingi Msasani na Uhuru Mchanganyiko zilizopo mkoa wa Dar es Salaam, shule za msingi Boma na Usa-River zilizopo mkoa wa Arusha pamoja na shule ya msingi Ruangwa iliyopo Lindi pamoja na” alisema Dokta Kimei.

Akizungumza kuhusu msaada huo wa shilingi milioni mia moja, Dokta Kimei alisema kuwa anaamini msaada huo utafanikisha ununuzi wa jumla ya mifuko 10,000 ya saruji ambayo itasaidia kujenga jumla ya vyumba vya ofisi za walimu 40 katika mkoa wa Dar es Salaam. “Kifupi ni kuwa benki ya CRDB, leo inajitolea kujenga majengo 40 ya ofisi za walimu wa mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Dkt. Kimei.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa Benki ya kizalendo yenye kujali mahitaji halisi ya wananchi.

“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, napenda kuishukuru kwa dhati kabisa Benki ya CRDB kwa msaada huu mkubwa na kwa kuendelea kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine hapa nchini. Msaada huu wa shilingi milioni 100 waliotupa leo, unatusogeza karibu zaidi na ndoto yetu ya kujenga ofisi nyingi za walimu mkoani kwetu ili kujenga mazingira bora ya kazi kwa walimu wetu na hivyo kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watoto wetu” alisema Mkuu wa Mkoa.

Akizungumzia hali ilivyo hivi sasa, Mheshimiwa Makonda alisema “Sote tunajua ni jinsi gani walimu wamekuwa wakikosa motisha ya ufanyaji kazi kutokana na mazingira magumu wanayokumbana nayo. Msaada huu unatupa faraja kubwa sana ya kuwa zipo taasisi za kizalendo kama Benki ya CRDB zinazoguswa na changamoto zinazotukabili. Naomba nikuhakikishie Dokta Kimei ya kuwa msaada huu utaenda kufanya kazi iliyokusudiwa”.

Mheshimiwa Makonda pia aliwasihi wadau wengine kuendelea kuchangia zoezi hilo kupitia akaunti maalum ya uchangiaji wa ujenzi wa ofisi hizo yenye nambari “0150296180200” iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam.

Maelezo jinsi ya kuchangia Ujenzi Ofisi za walimu Jijini Dar es Salaam:
Michango yote itumwe kwenye akaunti nambari iliyopo katika “0150296180200” iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam.

Njia za kuchangia:
  • Kupitia tawi lolote la Benki ya CRDB lililo karibu naw
  • Kupitia Huduma ya SimBanking kwa kupiga *150*03# na kisha kufuata maelekezo ya kuhamisha fedha
  • Kupitia Mawakala wote wa FahariHuduma wa Benki ya CRDB waliopo chi nzima
  • Kupitia kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti za mitandao yasimu na kupeleka kwenye akaunti 0150296180200 ya Benki ya CRDB


Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Jina
Namba ya Simu
Barua Pepe
Tully Esther Mwambapa
+255 769 200 600
Godwin Semunyu
+254 784 002020


No comments:

Post a Comment