Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi.
Mshindi wa Januari 2015 wa shindano la wazo la biashara 3N anatarajiwa kutangazwa siku ya Alhamisi ya Februari 12 kuanzia saa tano asubuhi jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Dk. Reginald Mengi kupitia kurasa wake wa twitter, alitangazia umma kuwa Shindano hilo jipya lijulikanalo kwa kifupi -3N, ikiwa ni kifupisho cha ‘Nitabuni wazo la biashara, Nitatekeleza, na Nitafanikiwa’, ambapo mshindi wa kwanza wa mwezi Januari anatarajiwa kutangazwa siku hiyo ya alhamisi Februari 12.
Dk. Mengi aliweka ujumbe huo twittter : “Kutokana na sababu zisizozuilika mshindi wa Januari wa shindano la 3N atatangazwa Februari 12 saa 5 asubuhi. Samahani kwa usumbufu wowote”.
Kwa mujibu wa Dk. Mengi awali mshind I alitakiwa kutangazwa Jumatano ya leo ya Februari 11, kabla ya kusogeza mbele hiyo Februari 12.
Shindano hilo litakuwa linafanyika kila mwezi kwa muda wa miezi sita kuanzia Januari Mosi 2015, hadi Juni 30, 2015, na mshindi wa kila mwezi atajishindia ruzuku ya shilingi milioni 10 atakazozitumia kutekeleza kwa vitendo wazo lake la biashara.
Shindano hilo, linawashirikisha Watanzania pekee, litaendeshwa kwa njia ya mtandao wa kompyuta ambapo mshiriki atatuma wazo lake la biashara kwa anuani ya twita @regmengi Shindano la Wazo la Biashara. Katika mchujo wa kwanza jopo la wataalamu litateua mawazo 10 bora Zaidi na waliotoa mawazo hayo watafanyiwa usaili kwa njia ya simu ili jopo hilo lijiridhishe kama mawazo waliyoyotuma ni yao binafsi, na kama wamejipanga vizuri kutekeleza kibiashara.
Kutokana na mawazo hayo 10 teule, jopo litachagua wazo moja kuwa mshindi. Hii ni mara ya tatu kwa Dkt. Mengi kuendesha shindano kwa kutumia mtandao wa kompyuta wa twitter kwa kuamini kwake kuwa mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa katika kuchochea ujasiriamali hasa kwa kizazi cha sasa.
Shindano la kwanza na la pili lililoendeshwa mwaka jana lilikusudiwa kushawishi mawazo ya kuondoa umaskini katika taifa lenye utajiri mkubwa, lakini watu wake wengi wakiwa bado wametopea katika lindi la umaskini.
Awali akizungumza katika uzinduzi wa shindano hilo, Dkt. Mengi alisema shindano hilo limelenga kuhimiza watu kuwa na upeo mkubwa wa kuona fursa za kibiashara na kuzitumia kujikwamua kiuchumi. Pia alisema shindano hilo ni mchango wake binafsi wa kuunga mkono jitihada za serikali na sekta binafsi za kuwakomboa wananchi kiuchumi kwa njia za ujasirimali, kwani amesema Sera zote mbili za kitaifa za Elimu ya juu na maendeleo ya viwanda vya kati na vidogo zina vipengele vya kuchochea na kuendeleza utamaduni wa ujasirimali wa mtu mmoja mmoja.
“Kwa muda mrefu nimekuwa nikishawishi uwepo wa moyo wa ujasirimali miongoni mwa wa Watanzania na hasa kwa vijana. Ni ndoto yangu kuona uchumi wetu unakua kwa kasi kiasi cha kuzalisha zaidi ya mamilionea 100 kila mwaka wanaoendesha biashara halali,” alisema.
Alisema kuwa na wazo sahihi la biashara, katika muda muafaka na eneo sahihi ni muhimu zaidi kuliko ruzuku ya fedha.
“Nataka vijana watambue kwamba wanaweza kuanza na kitu kidogo na kukua kufikia kampuni kubwa kabisa ya kimataifa unayoweza kufikiria,” alisema na kusisitiza kwamba anaamini siku moja mazingira ya ujasirimali nchini Tanzania yakuwa miongoni mwa mazingira bora kabisa barani Afrika.
Amesisitiza kuwa Shindano hilo liko wazi kwa watanzania wote na wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanapeleka wazo lao la biashara kwa Dk Mengi kupitia mtandao wa kompyuta wa twita, kwa kumtag Dk Mengi kwenye @regmengi.
Aidha amesema ni wale tu watakaomtag ndio watafikiriwa na jopo la wataalamu, na kusisitiza kuwa maamuzi ya jopo la Wataalamu yatakuwa ni ya mwisho.
Washindi wa kila mwezi wataarifiwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi kwa kupitia akaunti zao za twita (DM) na kupewa ruzuku yao katika sherehe fupi itakayohudhuriwa na waandishi wa habari.
Na Andrew Chale wa modewjiblog
No comments:
Post a Comment