Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Saturday 28 February 2015

WAZIRI WA UJENZI MHESHIMIWA DKT. JOHN MAGUFULI AKAGUA KIVUKO CHA MV DAR ES SALAAM

Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiwaita wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika eneo la Ferry kwa ajili ya safari ya kwenda Bagamoyo na kurudi kwa safari ya majaribio kwa kutumia kivuko cha MV Dar es Salaam alichokikagua jana.
Kivuko cha MV Dar es Salaam kikiwa njiani kuwasili eneo la Magogoni kwa ajili ya kuanza safari ya kwanza ya majaribio ya kwenda Bagamoyo mkoani Pwani. Kivuko hiki kinauwezo wa kubeba abiria zaidi ya 300.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakipanda kivuko cha MV Dar es Salaam kwa ajili ya Safari ya majaribio ya kwenda Bagamoyo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo akimpokea Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuwasili Bagamoyo na Kivuko cha MV Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Raymond Mushi kushoto wakiwa safarini kuelekea Bagamoyo Mkoani Pwani, akiwa na Kamanda wa Navy, Meja Jenerali Rogastian Laswai.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliopata fursa ya kupanda kivuko hicho wakitazama madhari ya jiji wakati wakiwa safarini.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amekagua kivuko cha MV Dar es salaam kinachotarajia kutoa huduma zake kati ya Dar es salaam na Bagamoyo na kuahidi kuwa kivuko hicho kitaanza kazi siku chache zijazo mara baada ya kukamilika kwa vituo vya maegesho.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Waziri Magufuli amewataka wakazi wa Dar es salaam na Bagamoyo kukitumia kivuko hicho ambacho kitawawezesha kufika katika maeneo yao kwa haraka na kuepuka usumbufu wa msongamano katikati ya jiji la Dar es salaam.

“Tumieni kivuko hiki kwa uangalifu ili kidumu kwa muda mrefu, na sisi Serikali tutahakikisha tunaweka nauli nafuu ili kuwezesha wananchi wengi kumudu kutumia usafiri wa kivuko hiki, amesema Waziri Magufuli”.

Waziri Magufuli amemtaka mkandarasi wa Ujenzi wa maegesho ya kivuko hicho ambae ni Kamandi ya Wanamaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kukamilisha ujenzi wa maegesho ya kivuko hicho mapema iwezekanavyo ili huduma za usafirishaji zianze mara moja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndikilo ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuwezesha kupatikana kwa kivuko cha MV Dar es salaam ambacho kitafungua fursa za kiuchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Aidha, Eng. Ndikilo ameiomba Wizara ya Ujenzi kuiendeleza barabara ya Bagamoyo- Zinga hadi Mbegani na kuhakikisha kuwa na usafiri wa basi moja kutoka Bagamoyo kwenda Mbegani na kuwepo maegesho ya magari yenye usalama.

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) Eng. Marceline Magessa, amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya kuanza kazi kwa kivuko hicho yamekamilika ambapo tayari manahodha, mabaharia na mafundi watakaohudumia kwenye kivuko hicho wameshaajiriwa.

Aidha Eng. Magessa alibainisha kuwa Kivuko cha MV Dar es salaam kimetengenezwa na kampuni ya Western Marine Shipyard kutoka Denmark kwa takriban Shilingi bilioni 8 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 wakiwa wamekaa.

Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji ya JWTZ Meja Jenerali Rogasian Laswai, amemshukuru Waziri kwa kupewa kazi ya kujenga maegesho hayo na kuahidi kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ili wananchi wanufaike na huduma za kivuko hicho mapema.

Takriban vituo saba vinatarajiwa kujengwa kwa ajili ya maegesho ya kivuko hicho ikiwemo Magogoni, Kawe, Jangwani, Rungwe Oceanic, Mbweni, Kaole na Mbegani.


IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, WIZARA YA UJENZI

No comments:

Post a Comment