Dar es Salaam, Julai 1, 2026 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, imekabidhi rasmi kombe la ubingwa wa msimu wa 2025/26 kwa mabingwa wapya, Yanga SC, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya soka na sekta ya michezo nchini.
Hafla hiyo ya kihistoria ilifanyika katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo baada ya Yanga kuhitimisha msimu kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania, matokeo yaliyowapa pointi 75 na kuwatangaza mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa mara ya tano mfululizo. Simba SC ilimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 73 baada ya kuifunga KMC FC bao 1-0 katika mchezo wake wa mwisho wa msimu.
Mbali na kuwapongeza mabingwa hao, NBC ilitumia hafla hiyo kuwashukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), vilabu, wadau wa habari na matangazo ya mchezo huo, mashabiki na wadau wote wa soka kwa mchango wao mkubwa ulioifanya Ligi Kuu ya NBC kuendelea kukua na kuwa moja ya ligi zenye ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hafla ya kukabidhi kombe ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, Rais wa TFF Wallace Karia, Mwenyekiti wa TPLB Nassor Idrissa, Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Rayson Foya aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited Patrick Kahemele pamoja na viongozi mbalimbali wa soka na wadau wa michezo.
Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkuu wa Masoko wa NBC, David Raymond, alisema benki hiyo inajivunia kushuhudia ukuaji wa kiwango cha ushindani wa Ligi Kuu ya NBC tangu ilipoanza kuidhamini, akieleza kuwa ushindani huo umeongeza ubora wa mchezo, kuvutia mashabiki wengi zaidi na kuongeza thamani ya soka la Tanzania.
"Tangu tulipoanza kuidhamini Ligi Kuu ya NBC, tumeshuhudia ongezeko kubwa la ushindani na ubora wa mchezo. Kila msimu umekuwa wa kipekee na wenye mvuto mkubwa kwa mashabiki. Hii ndiyo sababu tunaendelea kujivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya soka la Tanzania," alisema Raymond.
Aliongeza kuwa NBC itaendelea kuongeza thamani ya udhamini wake kwa kuanzisha programu zitakazowanufaisha moja kwa moja wadau wa mchezo huo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuchochea maendeleo ya michezo sambamba na ukuaji wa uchumi.
Kwa mujibu wa Raymond, maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na maendeleo ya soka la vijana, mafunzo ya wachezaji, huduma za bima hususan bima ya afya kwa wanamichezo, pamoja na utoaji wa huduma za kifedha zinazolenga kuwawezesha wachezaji na taasisi za michezo kujijengea utulivu wa kifedha na kufanikisha malengo yao ya muda mrefu.
"Tunaamini michezo ni sekta muhimu ya uchumi. Ndiyo maana tunaendelea kubuni suluhisho za kifedha zitakazowasaidia wanamichezo, vilabu na wadau wengine kujenga mustakabali imara wa kiuchumi sambamba na mafanikio yao uwanjani," alisisitiza.
Moja ya vivutio vikubwa vya siku hiyo ilikuwa namna kombe la ubingwa lilivyowasilishwa. NBC iliandaa helikopta maalum iliyobeba kombe hilo na kulizungusha katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wakati michezo ya mwisho ya ligi ikiendelea, ikisubiri kujulikana kwa bingwa kutokana na ushindani mkali uliokuwepo kati ya Yanga na Simba, zilizotenganishwa na pointi mbili pekee kabla ya mechi za mwisho.
Baada ya Yanga kuthibitisha ubingwa wake kwa ushindi dhidi ya JKT Tanzania, helikopta hiyo ilitua katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kukabidhi kombe rasmi kwa mabingwa wapya, tukio lililoibua shamrashamra zaidi kutoka kwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia historia hiyo.
Katika kuendeleza uzoefu wa wadau wa ligi, NBC pia iliwawezesha baadhi ya wateja wake na maofisa wa benki hiyo kuhudhuria michezo ya mwisho wa msimu kwa kuandaa usafiri maalum kwenda katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na KMC Complex, ambako Simba iliifunga KMC bao 1-0.
Udhamini wa NBC katika Ligi Kuu umeendelea kuonekana kama moja ya uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi katika michezo nchini, ukiwa si tu chanzo cha kukuza ushindani wa soka bali pia ukifungua fursa za kiuchumi kwa vilabu, wachezaji, wadau wa biashara na mashabiki, hatua inayochangia maendeleo ya uchumi wa michezo nchini.



No comments:
Post a Comment