Dar es Salaam — Benki ya NMB imeandika historia mpya katika sekta ya huduma za kifedha nchini Tanzania baada ya kuwa benki ya kwanza kuzindua teknolojia ya kisasa ya malipo ijulikanayo kama "NMB TAP Wearables".
Huduma hii bunifu inamwezesha mteja kufanya malipo kwa urahisi, haraka na usalama wa hali ya juu kupitia vifaa vinavyovaliwa (wearables) ikiwemo pete, bangili na stika maalum, bila hitaji la kubeba pesa taslimu au kadi.
Uzinduzi Wafanyika Dar es Salaam
Uzinduzi wa NMB TAP Wearables umefanyika jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha na teknolojia, akiwemo Meneja Biashara wa Mastercard Tanzania, Moses Alphonce, aliyeipongeza NMB kwa kuendelea kuongoza katika bunifu za huduma za kifedha nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Wawekezaji, Uendelevu na Mawasiliano wa NMB, Innocent Yonazi, alieleza kuwa NMB TAP ni taswira halisi ya mustakabali wa huduma za kibenki nchini Tanzania.
“NMB TAP ni ‘future of banking in Tanzania’. Kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea pesa taslimu na kadi, lakini sasa tunaelekea katika suluhisho za kisasa zinazoendana na kasi ya maisha ya kidijitali,” alisema Yonazi.
Aliongeza kuwa lengo la NMB ni kumweka mteja katikati ya ubunifu, kwa kutoa huduma zilizo rahisi kutumia, salama na zenye kuokoa muda, huku zikiondoa usumbufu wa kubeba pochi, mikoba au ‘wallet’.
Mapinduzi ya Malipo ya Kidijitali
Yonazi alisisitiza kuwa kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya NMB na Mastercard, benki hiyo imelenga kuleta mapinduzi makubwa katika mifumo ya malipo nchini, kwa kumpa mteja huduma ambayo haijawahi kuwepo hapo awali.
“Kupitia NMB TAP, tunamuwezesha mteja kufanya malipo kwa haraka na usalama wa hali ya juu, bila kuwa mtumwa wa mifumo ya kizamani ya kibenki,” aliongeza.
Mastercard Yapongeza Ubunifu wa NMB
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Mastercard Kanda ya Afrika Mashariki, Shehryar Ali, aliipongeza NMB kwa kuendelea kuwa kinara wa ubunifu unaolenga kutatua changamoto za wateja wa benki.
“Kila mwaka NMB imekuwa mstari wa mbele kuanzisha huduma bunifu zinazokuja kuigwa na taasisi nyingine za kifedha. NMB TAP ni huduma ya kihistoria na ya kwanza kabisa nchini Tanzania,” alisema Ali.
Alieleza kuwa NMB TAP ni huduma salama zaidi, isiyotumia ‘password’, hivyo kuondoa kabisa mianya ya uhalifu wa kifedha, wizi wa taarifa za akaunti na udanganyifu wa kimtandao.
“Hakuna uwezekano wa kudukuliwa au kuibiwa taarifa za akaunti ya mteja. Usalama wa mteja umepewa kipaumbele cha juu,” alisisitiza.
Safari ya Mageuzi ya NMB
Naye Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alielezea safari ya mageuzi ya kimfumo ya benki hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997.
“Tulianza na ‘pass book’, tukafika kadi ya njano mwaka 2006, ushirikiano na Mastercard mwaka 2014, hadi kufikia huduma za ATM, POS, Lipa Mkononi, QR Code, QR Pay by Link, na sasa tunafungua ukurasa mpya kupitia NMB TAP,” alisema Mponzi.
Alibainisha kuwa NMB TAP Wearables ni hatua kubwa ya kimapinduzi katika historia ya benki hiyo, na akawahimiza wateja kuanza kuomba huduma hiyo mapema ili kunufaika na teknolojia ya kisasa ya malipo.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment