Dodoma, 16 Septemba 2024: Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bw Theobald Sabi, amesisitiza umuhimu wa teknolojia, elimu kwa umma pamoja na ubia baina ya wadau muhimu wa sekta ya bima ikiwemo serikali, taasisi za fedha na kampuni za mitandao ya simu kama suluhisho muhimu katika kuimarisha na kuchochea kasi ya upatikanaji wa huduma ya bima jumuishi nchini.
Akiwasilisha mjadala wake kuhusiana na mada "Bima Jumuishi: Bidhaa Bora na Usambazaji Kupitia Teknolojia," wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Bima mwaka 2024 jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Sabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) alisisitiza kuhusiana na matokeo ya ukuaji wa teknolojia yanavyoweza kuchochea mabadilliko chanya kwenye sekta hiyo.
Kilele cha maadhamisho hayo kilihusisha kongamano maalum la wadau mbalimbali wa sekta ya bima nchini, likiongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, sambamba na Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware na Naibu wake Bi Khadija Said pamoja na Balozi wa Bima Tanzania ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Saidi.
"Kwa kuwa ni asilimia 10 tu ya Watanzania wanatumia huduma za bima (Finscope, 2023), ipo haja ya kutegemea teknolojia kama suluhisho muhimu katika kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hii muhimu. Ubunifu hauishii tu kukidhi mahitaji ya wateja bali pia unaongeza upatikanaji wa bidhaa za bima, kuimarisha usambazaji, kudhibiti utapeli, na kudhibiti vihatarishi,’’ alisema.
Zaidi, Sabi alitaja baadhi ya changamoto kubwa katika ukuaji wa sekta ya bima nchini ikiwemo vipato duni, wananchi kutokuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba, na mtazamo hasi wa umma kuhusu bidhaa za bima. Ili kukabiliana na changamoto hizi, Sabi alipendekeza suluhisho mbalimbali ikiwemo ongezeko la utoaji elimu ya kifedha na uanzishwaji wa huduma za bima nafuu zinazozingatia mahitaji ya makundi ya watu wenye vipato vya chini.
"Kwa kufuata njia ya teknolojia, hasa kupitia majukwaa ya simu, matumizi ya taarifa sahihi katika kufanya maamuzi na kuongeza ushirikiano na wadau wengine wakiwemo mawakala kama NBC Wakala, itasaidia sana kutoa huduma za bima katika maeneo ya vijijini yenye uhitaji mkubwa. Mifano yenye mafanikio kama vile Vodabima ya Vodacom Tanzania na NIC Kiganjani ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) inathibitisha ufanisi wa huduma za bima kupitia simu katika kuongeza upatikanaji wa huduma hii muhimu" alibainisha.
Akitumia uzoefu wa Benki ya NBC, Sabi alielezea namna benki hiyo ilivyo na mchango mkubwa katika kuchochea ukuaji wa sekta ya bima nchini. "Kama benki tunajivunia kuwa mdau mkuu katika sekta ya huduma za bima kupitia benki (bancassurance’) nchini, na kuchangia asilimia 18.3 ya malipo ya bima yaliyorekodiwa (GWP) na kuendesha asilimia 45.7 ya malipo ya bima ya maisha katika kipindi cha miaka minne iliyopita.’’
“Jitihdaza zetu kama vile huduma ya bima ya mazao kwa wakulima wa tumbaku na bima ya Afya kwa wakulima yaani ‘Wakulima Afya’ kwa zaidi ya wakulima 200 katika maeneo ya Lindi, Masasi na Mtwara, zinathibitisha kujitolea kwetu katika kusaidia sekta ya kilimo.’’
"Mtandao wetu wa mawakala, unaojumuisha zaidi ya mawakala 16,000 kote nchini, una jukumu muhimu katika kuongeza upatikanaji wa huduma ya bima, hasa katika jamii za vijijini. Tumepanga kuwajengea uwezo mawakala 3,000 zaidi ifikapo mwaka 2028 ili kuimarisha mtandao wetu wa usambazaji." aliongeza.
Ili kusaidia mawakala hao, Sabi alisema benki hiyo imeweka mifumo ya kisasa dhidi ya udanganyifu na suluhisho za teknolojia ya simu, kama vile programu ya Policy Pro, inayorahisisha uendeshaji wa huduma hizo na kuhakikisha usimamizi wa kisheria.
Akizungumza kama Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) Sabi alithibitisha kujitolea kwa chama hicho katika kusaidia ukuaji wa sekta ya bima nchini.
"Bima jumuishi si uwezekano tu bali ni dharura. Kwa kufanya kazi pamoja, benki, kampuni za bima, watoaji wa huduma za teknolojia na serikali, tunaweza kuunda mfumo imara ambao utasaidia upatikanji wa huduma ya bima kwa watanzania wote, bila kujali mahali walipo au hadhi yao ya kiuchumi," alihitimisha.
No comments:
Post a Comment