Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Zanzibar Ramadhan Lesso (pichani) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya utambulisho wa huduma ya kidigitali ya ‘NBC Connect’. |
Mkuu wa Miamala na Amana za Wateja Wakubwa wa NBC, Jimmy Myalize (pichani) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya utambulisho wa huduma ya kidigitali ya ‘NBC Connect’. |
Baadhi ya wateja wa benki ya NBC pamoja na maofisa wa benki hiyo wakifuatilia utambulisho wa huduma ya kidigitali ya ‘NBC Connect’. |
Hafla ya utambulisho wa huduma hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki Zanzibar ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi-Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji. Hafla hiyo pia ilihusisha uwepo wa wateja wa benki hiyo visiwani humo, huku wafanyakazi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na wateja wa serikali Benki ya NBC Linley Kapya.
Akizungumza kwenye tukio hilo lilidumu kwa siku tatu ambalo ni muendelezo kufuatia matukio kama hayo yaliyofanyika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa, Kapya alisema huduma hiyo ya kidigitali ni uthibitisho wa dhamira ya benki hiyo kuwapatia wateja wake huduma bora za kibenki ambazo ni rahisi, salama na zinazofaa na kukidhi mahitaji ya wateja.
“Kinachofanyika leo ni utambulisho rasmi wa huduma hii kwa kuwa tayari wateja wetu wameshaipokea huduma hii na wanaifurahia. Tupo hapa kupata mrejesho na kutoa ufafanuzi kwenye maeneo muhimu ili waweze kuifurahia huduma hii kwa upana wake. Ikitumika vizuri huduma hii, wateja wetu wenye makampuni na taasisi mbalimbali zilizopo visiwani Zanzibar watapata fursa na uwezo wa kufanya miamala yao ya kifedha kwa urahisi zaidi na kupata uzoefu mpya katika kupata huduma za kibenki.’’ Alisema.
Akiizungumzia huduma hiyo, Dkt. Mngereza alisema imesaidia kuleta mapinduzi mapya katika utoaji wa huduma za kibenki huku ikichochea kasi ya ukuaji uchumi kupitia urahishwaji wa malipo na ukusanyaji wa mapato mbalimbali yakiwemo ya serikali.
“Utambulisho wa huduma hii ya NBC Connect hapa Zanzibar unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia huduma bora za kifedha na uchumi jumuishi. Kupitia huduma hii mashirika na taasisi mbalimbali zitaweza kufanya malipo kwa wakati bila usumbufu na kwa kuwa ni rahisi kwa huduma hii kuwafikia walengwa kwa wingi wao basi pia itachagia ukuaji wa uchumi…naomba sana mashirika, taasisi na kampuni mbalimbali hapa Zanzibar waipokee huduma hii,’’ alisema
Akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo Mkuu wa Miamala na Amana za Wateja Wakubwa wa NBC, Bw Jimmy Myalize alisema huduma hiyo inawapa wateja uwezo wa kufanya miamala kirahisi popote, wakati wowote ikiwemo kufanya malipo ya ndani na nje ya nchi, malipo ya serikali pamoja na malipo kwa mkupuo bila kutumia muda mrefu kwa kutumia tu simu au kompyuta.
“Wateja pia wataweza kupata taarifa za miamala waliyofanya popote pale walipo pasipo kulazimika kwenda benki. Huduma hii imetengenezwa kwa teknalojia ya kisasa na yenye usalama wa hali ya juu ambayo imezingatia na kutoa kipaumbele kwenye usiri wa taarifa za mteja. Ubunifu wa huduma hiyo huakikisha taarifa za kifedha za wateja zinalindwa wakati wote.’’ Aliongeza.
Aliongeza kuwa pamoja na huduma hiyo benki hiyo imejipanga kutoa usaidizi binafsi kwa wateja kupitia kituo chake cha huduma kwa wateja ambapo wataalamu wa huduma hiyo wamejipanga kuwasaidia wateja kulingana na mahitaji yao na kutoa mwongozo wa jinsi ya kutumia jukwaa hilo kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment