Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday 2 February 2023

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC) LAPATA FAIDA, UKWASI WAZIDI KUKUA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu akizungumza na vyombo vya habari NHC Kambarage House Jijini Dar e Salaam jana.
  • Mkurugenzi Mkuu asisitiza kusimamia nidhamu ya utendaji kazi ndani ya Shirika
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepata faida kabla ya kodi na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 92.9 ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemiah Kyando Mchechu alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari NHC Kambarage House Jijini Dar es Salaam. Lengo na Mkutano likiwa ni kuelezea mafanikio na mizania ya Shirika kwa mwaka 2021/2022 na kuelezea mwelekeo wa Shirika kwa Mwaka 2023.

“Shirika limeendelea kuongeza faida kabla ya kodi na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 92.9 (2021: faida ya TZS 93,966 bilioni). Aidha, mwaka 2020/2021 faida ilishuka kutokana na kushuka kwa hali ya soko la nyumba nchini,” Alisema Mchechu.

Alisema kuwa hata hivyo, faida halisi inayotokana na shughuli za Shirika iliongozeka hadi kufikia shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/2022 kutoka shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020/21. Ongezeko hili lilienda sambamba na ongezeko la majengo.

Amesema kwamba hali ya soko la nyumba imeanza kuimarika na kwamba ni matarajio ya Shirika kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 litaendelea kupata faida kubwa.

Kuhusu Mapato amesema kuwa Shirika limeendelea kuongeza mapato yake hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 257.47 mwaka 2022 (2021: mapato ya TZS 144.42 bilioni). Mwaka 2021/2022, mapato ya kodi yamepanda na kufikia shilingi bilioni 90.76 kutoka shilingi bilioni 89.23 mwaka 2020/2021.

Kuhusu mapato ya mauzo ya nyumba amesema kuwa yamepanda kutoka Shilingi bilioni 29.33 mwaka 2020/21 na kufikia shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/22. Vilevile, mapato ya miradi ya Ukandarasi yamekua kutoka shilingi bilioni 25.60 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 43. 98 mwaka 2021/22.

Amesema mizania ya Shirika imeendelea kuimarika na thamani ya mali za Shirika (Total Assets) kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kuwa hadi kufikia Juni 31, 2022 zilikuwa shilingi trilioni 5.04.

“Mizania hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka kwa wastani wa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019. Thamani hii inahusisha vitega uchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na Shirika ambayo bado haijaendelezwa ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea,”Alisema Mchechu.

Mchechu alitaja vipaumbele kumi vya Shirika, miongoni mwa vipaumbele hivyo vikiwa Shirika kuendelea kukamilisha ujenzi wa miradi iliyokuwa imesimama ikiwemo mradi wa Morocco square ambao ujenzi wake upo kwenye hatua za mwisho kukamilika. Mradi huu unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023.

Pia amesema kuwa Shirika litaendelea na utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika maeneo mbalimbali nchini na limeanza na ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam na litaanza ujenzi wa nyumba 240 eneo la Medeli Jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza. Programu ya nyumba za Samia Housing Scheme (SHS) umelenga kutatua changamoto ya makazi bora kwa watu wa kipato cha chini na kati.

Ametangaza pia kuwa Shirika litaanza ujenzi wa Shopping Mall ya kisasa Jijini Dodoma ili kuweza kuwapa wakazi wa Jiji hilo eneo zuri na kubwa la kujipatia huduma mbalimbali za kijamii. Pia Shirika litaendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia shilingi bilioni 21 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia takriban shilingi bilioni 11. Msisitizo utakuwa kuhakikisha kuwa kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha Shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali hizi za umma;

“Tutaendelea kusimamia nidhamu ya utendaji kazi ndani ya Shirika ili kuweza kuamsha ari na tija kwa Watendaji. Huduma bora kwa wateja ndiyo kipaumbele cha utendaji wa watumishi wa Shirika,”Alisema Mchechu.

No comments:

Post a Comment