Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Friday, 16 July 2021

KAMPUNI YA DAVIS & SHIRTLIFF YAKABIDHI BOMBA LA MAJI LINALOTUMIA NISHATI YA JUA KWA WAKAZI WA KIMBIJI

Mwanamke wa Kijiji cha Kizito Wonjwa akiwa amebeba maji aliyochota kutoka bomba jipya la maji mara baada ya kukabidhiwa. Nyuma ni Afisa Tarafa wa Pemba Mnazi, Florence Msigwa, viongozi wa mitaa, wafanyakazi wa D&S na wakazi wa Kijiji wakifurahia.
Afisa Tarafa wa Pemba Mnazi, Florence Msigwa akiwa amebeba ndoo ya maji mara baada ya kupokea na kuzindua bomba lililokabidhiwa na kampuni ya D&S siku. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa D&S Tanzania, Benjamin Munyao na Diwani wa Kata ya Kimbiji Bwana Sanya Muhdin.
Afisa Tarafa wa Pemba Mnazi, Florence Msigwa akiwa ameshika mkasi baada ya kukata utepe akiwa anazindua bomba la maji la kisasa. Kulia kwake ni Diwani wa Kimbiji, Sanya Muhdin, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kizito Wonjwa, Juma Kizengo na Mhandisi kutoka Africabo, Osca Mwishee. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa D&S Tanzania Bwana Benjamin Munyao na wafanayakazi wenzake wakifurahia uzinduzi wa bomba.

Dar es Salaam - Kampuni ya Davis & Shirtliff (D&S) Group, inayohusika na usambazaji na uuzaji wa vifaa vya maji nchini Tanzania imekabidhi kituo cha maji kinachotumia nishati ya jua kujiendesha kwa wakazi wa kata ya Kimbiji wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

Bomba hilo lililogharimu takribani Shilingi Milioni 7, limejengwa na Kampuni ya Davis & Shirtliff Group na Africabo Ltd na linahudumia zaidi ya kaya 150 za kijiji cha Kizito Wonjwa na wakazi wengine wa karibu.

Kampuni ya Africabo ilichimba kisima chenye kina cha mita 35, wakati D&S imeweka mashine ya kusukuma maji ambayo hujiendesha kwa kutumia nishati ya jua na kuweka tanki la mita 300 kwa ajili ya kuhifadhi maji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bomba, ilifanyika katika kijiji cha Kizito Wonjwa mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa D&S, Benjamin Munyao alisema, mashine iliyowekwa inawasaidia wakazi hao kuchota maji bila kutumia mikono yao kusukuma bomba.

"Mtambo huu unaotumia nishati ya jua, una uwezo wa kusukuma lita 500 hadi lita 1000 za maji kwa saa. Mfumo wa nishati ya jua pia unarahisisha kituo hicho kufanya kazi kwa masaa 24," alisema.

Bomba hilo ni ukombozi kwa wakazi wa kata ya Kimbiji ambao walikuwa wakitegemea visima vifupi ambavyo hukauka maji mara kwa mara.

Sanata Omary (30), mama wa watoto wanne, mkazi wa kijiji cha Kizito Wonjwa alisema kabla ya kujengwa bomba la kisasa, alikuwa akiamka saa 10 usiku, na kumuacha mumewe na watoto wamelala na kwenda kuchota maji. Bado wakati mwingine alikosa maji maana wanaoamka muda huo ni wengi.

"Kuoga ilikuwa ni jambo la hanasa sana kwetu. Watoto walilazimika kuosha uso tu kabla ya kwenda shule na kulala. Ilinibidi nitafute maji wakati wa usiku. Sikuweza hata kufurahia ndoa yangu," alisema.

Lakini kwa sasa ana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu D&S wamewezesha upatikanaji wa maji safi na salama ambayo yanakidhi mahitaji.

"Tulikuwa tukichimba visima vifupi kwa mikono, hivyo maji hayakuwa safi na salama kwa ajili ya kunywa na kupika. Hata hivyo, hatukuwa na chaguo lingine. Mlipuko wa magonjwa ulikuwa jambo la kawaida kwetu, hasa kwa watoto," alisema.

"Leo, mimi na familia yangu tunajisikia salama. Ninaweza kupata maji wakati wowote sasa, na natumia muda mwingi kufanya shughuli zingine za kimaendeleo pamoja kuitunza familia yangu. Hata ndoa yangu inafuraha sasa," aliongezea.

Viongozi wa serikali za mitaa akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kizito Wonjwa Juma Kizengo, Diwani wa Kata ya Kimbiji Sanya Muhidin na Afisa tarafa wa Pemba Mnazi Florence Msigwa waliishukuru sana Kampuni ya D&S kwa ujenzi wa bomba hilo la kisasa na kuahidi kulitunza.

Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Afisa Tarafa wa Pemba Mnazi, Bwana Msigwa aliahidi kutunza miundombinu hiyo ya maji na kuomba wadau hao wa maendeleo kuendelea kujenga visima na mabomba ya kisasa katika maeneo mengine yenye changamoto.

“Hivi karibuni, kumekuwa na wimbi la wizi wa sola hapa tarafani. Zaidi ya sola sita zimeibiwa ndani ya miezi miwili. Sasa ninatangaza msako mkali wa wezi hao ili kuhakikisha miundo mbinu ya maji kama hii inalindwa na kuwanufaisha wananchi wote,” alisema.

No comments:

Post a Comment