Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday 19 July 2018

BENKI YA BIASHARA YA DCB YATANGAZA UKUAJI WA FAIDA WA ZAIDI YA ASILIMIA 100 KWA NUSU YA MWAKA 2018

Mkuu wa Idara ya Fedha wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati benki hiyo ikitangaza faida ya shs bilioni 1.0 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2018. Kulia ni Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Rahma-Gemina Ngassa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Deogratias Thadei.
Dar es Salaam; Julai 19, 2018 - Benki ya biashara ya DCB (DCB Commercial Bank Plc) imetangaza kupata faida ya sh. bilioni 1.0 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018 kilichoishia mwezi Juni, ikiwakilisha ongezeko la asilimia 106 kutoka faida ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2017. Utendaji wa benki umeimarika ikilinganishwa na miaka miwili iliyotangulia huku ufanisi katika nyanja zote muhimu ukiongezeka kwa kiwango cha kuridhisha.

Aidha, ongezeko hilo la faida, pia lilipatikana kupitia kuimarika kwa mapato yatokanayo na riba pamoja na yale yasiyotokana na riba na limechagizwa na mkazo wa benki katika amana za gharama nafuu, usimamizi wa mizania wenye ufanisi, ufunguaji wa tawi la Dodoma na vituo vya huduma (service centers), ukuaji wa mfumo wa kibenki wa kidijitali na wa mawakala pamoja na ongezeko la wateja na miamala.

Mafanikio haya, pia yametokana na ukuaji wa mikopo ambapo benki imefanikiwa kuongeza kiwango cha mikopo kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mikopo iliyokuwepo katika mwezi Desemba 2017. Kwa kuongezea, ufanisi wa benki hii umeongezeka hasa katika usimamizi wa matumizi ya riba na yasiyo ya riba, ufanisi wa mizania pamoja na uboreshaji wa huduma za utoaji wa mikopo.

Katika utoaji huduma, benki ya biashara ya DCB imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wateja kufikia 191,133 katika nusu ya pili ya mwaka iliyoishia mwezi Juni 2018 kutoka 188,305 mwezi Desemba mwaka 2017. Ongezeko hili la wateja 2,828, limechangia kuimarisha mapato ya benki kupitia kuongezeka kwa miamala, amana za kudumu na utoaji mikopo.

Mikopo ghafi ya wateja iliongezeka kufikia shilingi bilioni 93.7 kufikia mwezi Juni mwaka 2018, kutoka shilingi bilioni 88.7 iliyokuwepo mwezi Desemba 2017, ambalo ni ongezeko la asilimia 5. Aidha, benki ya DCB imefanikiwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu kutoka asilimia 18.8 mwezi Desemba 2017 kufikia asilimia 17.7 katika nusu mwaka inayoishia mwezi Juni 2018. Upunguaji huu umechagizwa na ufanisi katika ukusanyaji wa madeni sugu, utoaji wa mikopo mizuri na kwa kuzingatia weledi, hali iliyoboresha ulipaji wa wateja.

Ili kuongeza ufanisi wa mizania, benki ilipunguza amana aghali kwa kiwango kikubwa na hivyo kusababisha amana za wateja kupungua katika nusu ya pili ya mwaka 2018 ikilinganishwa mwezi Desemba 2017. Upunguaji huu wa amana ghali umechangia kupungua kwa gharama za riba za amana na hivyo kuiwezesha benki kutoa mikopo nafuu Zaidi kwa wateja.

Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 (Ikijulikana kama Dar es Salaam Community Bank) kutokana na kilio cha wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam kutokuwa na namna ya kupata mitaji midogo ya biashara jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika jitihada za kuboresha biashara zao sambamba na masharti magumu kutoka kwa benki nyingi za kibiashara. Kwa kipindi chote cha miaka 16 ya uendeshaji, jukumu mama la benki hii limeendelea kuwa ni kutoa huduma bora za kifedha huku ikijikita zaidi katika kutengeneza miradi endelevu ya kupunguza umaskini na kuendeleza jamii.

Katika miaka yake takriban 16 ya uendeshaji, benki ya DCB imeweza kukuza idadi ya matawi kutoka tawi moja na kufikia manane (8) hadi mwaka huu wa 2018. Ukuaji huu umechangia benki kupata faida mfululizo tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2015, na imekuwa ikitoa gawio kwa wanahisa wake katika kipindi chote cha miaka 12. Hata hivyo, kutokana na changamoto za mpito, benki ilipata hasara katika miaka miwili ya 2016 na 2017, kabla ya kuzirekebisha na kurejea katika faida mwaka huu wa 2018.

Hapo mbeleni, benki ya DCB, ambayo imesajiliwa katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE), inatazamia kukuza mizania yake kwa kutumia fursa za ukuzaji biashara na ina azimia kutumia ipasavyo fursa na njia mbadala za utoaji huduma kwa wateja kupitia mitandao, wakala wa kibenki, na upanuzi wa mitandao ya matawi na vituo vidogo vya huduma (service centres) ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa utengenezaji wa mapato kupitia njia ya mapato yasiyo ya riba. Benki itaendelea kujiimarisha katika maeneo ambayo imefanya vizuri, huku ikiboresha huduma katika maeneo yenye uhitaji. Benki imepata mafanikio makubwa ambayo ni;
  1. Benki ya DCB ndio benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.
  2. Benki ya DCB ndio benki pekee iliyokua kutoka benki ya wananchi/jamii (community bank) na kufanikiwa kuwa benki ya biashara (commercial bank).
  3. Benki ya DCB imefanikiwa kukuza mtandao wa matawi yake kufikia manane huku ikifungua tawi Dodoma na inaendelea na mchakato wa kufungua matawi na vituo vya huduma (service centers) katika mikwa mingine.
  4. Benki ya DCB imefungua mtandao wa mawakala na huduma za kijiditali hadi kufikia mawakala zaidi ya 1,000 nchini nzima.
Kwa Mawasiliano;
Piga simu Namba: +255 22217201
Barua Pepe: info@dcb.co.tzau Tembelea www.dcb.co.tz

No comments:

Post a Comment