Foreign Exchange Rates

DStv Advert_010224

DStv Advert_010224

SBT Tanzania Advert_291123

Friday 27 October 2017

SERIKALI YAWEKA MSIMAMO WA KIBIASHARA EAC

Kwa ufupi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana wakati wa mjadala wa pamoja kuhusu mchango wa kampuni za kati na ndogo katika kufikia nchi ya viwanda na ushirikishaji wa wazawa.

Dar es Salaam. Serikali imesema haitakubali kuona bidhaa kutoka Tanzania zinazuiliwa kuingia katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki kwa sababu Mkataba wa Soko la Pamoja wa nchi hizo (EAC) unaruhusu kufanya biashara katika ukanda huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana wakati wa mjadala wa pamoja kuhusu mchango wa kampuni za kati na ndogo katika kufikia nchi ya viwanda na ushirikishaji wa wazawa.

Kabla ya mjadala huo, utafiti wa kampuni 100 za kati Tanzania uliwasilishwa kwa wadau na kubainisha changamoto mbalimbali ambazo kampuni hizo zinapitia katika ufanyaji wa biashara zao.

Shindano la kampuni 100 za kati limeandaliwa na Kampuni ya KPMG kwa ushirikiano na Mwananchi Communications Ltd (MCL) kupitia gazeti lake la The Citizen na tuzo zinatarajiwa kutolewa leo.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Research Solutions Africa umebaini kwamba theluthi mbili ya kampuni 4,000 zilizoshindanishwa zilionyesha nia ya kupanua biashara zao mpaka nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, zililalamikia upungufu wa mitaji ya kuziwezesha kupanua biashara zao. Pia, zimelalamikia utitiri wa kodi, jambo ambalo zilisema linaathiri mitaji yao na ufanyaji wa biashara nchini.

Profesa Mkenda aliwahakikishia wafanyabiashara hao kwamba Serikali imechukua hatua kumaliza sintofahamu ya kuzuiliwa kwa bidhaa za Tanzania zinazoingia Kenya na kusisitiza kwamba suala hilo likijirudia, itachukua hatua mara moja.

“Juhudi za viongozi wetu zimefanikisha kumaliza mgogoro ule, sitarajii kama utajirudia tena. Bidhaa za Tanzania zikizuiliwa tena tutachukua hatua, wanajua moto wetu. Kwa hiyo, wafanyabiashara wasisite kupeleka bidhaa zao nchi yoyote,” alisema Profesa Mkenda.

Kuhusu ujasiriamali, Profesa Mkenda alisema ni vyema vijana wakachukua jukumu hilo badala ya kuwaachia wazee ambao wakistaafu ndiyo wanakwenda kuanza ujasiriamali. Alisema hao hawawezi kufanya vizuri kama wale ambao wanaanza ujasiriamali wakiwa bado wadogo.

“Ni dhana potofu kufikiri kwamba ujasiriamali unatakiwa kufanywa baada ya kustaafu. Wafanyabiashara wakubwa waliofanikiwa walianza wakiwa bado vijana wadogo, wakawekeza muda wao kwenye biashara, ndiyo hao tunawaona sasa wakiwa na mafanikio makubwa,” alisema.

Mkurugenzi wa Resource Solutions Africa, Dk Jasper Grosskurth alisema asilimia 51 ya kampuni zilionyesha nia ya kupanua biashara kwenda Kenya wakati asilimia 38 zikitaka kwenda Uganda.

Hata hivyo, Dk Grosskurth alizitaka kampuni hizo kuwa na rekodi nzuri ya ulipaji wa kodi kwa sababu hiyo ni moja ya njia ya kujiongezea thamani na kuiwezesha kuhimili soko la ushindani.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tigo, Simon Karikari alisema maendeleo ya viwanda yanakwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia. Alisisitiza kwamba wao wakiwa ni wadau wa mawasiliano ya simu, wametoa fursa ya kurahisisha miamala kwa wajasiriamali.

Alisema wanawaunganisha wajasiriamali wakati wa kusambaza huduma zao kwa walaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisisitiza juu ya umuhimu wa sekta ya kilimo kwenye dhana nzima ya uanzishwaji wa viwanda akisema haviwezi kustawi kama kilimo kipo chini.

“Kutokana na umuhimu wa kilimo, ningependa kuona kauli mbiu yetu inaitwa ‘Tanzania ya kilimo na viwanda’ ili tusikiache kilimo nyuma wakati tunaelekea kwenye nchi ya viwanda,” alisema Nanai.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji wa Shirika la Viwanda Vidogovidogo (Sido), Titus Kyaruzi alisema ni muhimu kuwajengea uwezo vijana ili washiriki kwenye ujasiriamali.


Mwananchi

No comments:

Post a Comment