Kwa Ufupi
Kwenye taarifa yake ya awali iliyotolewa jana kwa wadau wake
na jamii kwa ujumla, kampuni hiyo imeeleza kuimarika kwa uzalishaji lakini
ikabainisha kupungua kwa mapato kutokana na zuio hilo lililoanza mapema Machi.
Dar es Salaam. Ikitarajia kuchapisha hesabu zake za fedha
kwa robo ya tatu ya mwaka, kampuni ya Acacia inaendelea kuugulia maumivu ya
zuio la kutosafirisha mchanga wa madini.
Kwenye taarifa yake ya awali iliyotolewa jana kwa wadau wake
na jamii kwa ujumla, kampuni hiyo imeeleza kuimarika kwa uzalishaji lakini
ikabainisha kupungua kwa mapato kutokana na zuio hilo lililoanza mapema Machi.
“Mauzo yalikuwa madogo kutokana na zuio la kusafirisha
makinikia yanayozalishwa kwenye migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi nchini
Tanzania,” inasema taarifa hiyo fupi.
Machi, Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini na
Rais John Magufuli akaunda kamati mbili za kuchunguza uchimbaji, usafirishaji
na biashara nzima ya dhahabu ambazo zilibaini udanganyifu unaofanywa hivyo
kulinyima Taifa mapato linayostahili.
Licha ya zuio hilo, Serikali ilifanya mabadiliko kwenye
sheria za madini ili kuongeza usimamizi wa uzalishaji, udhibiti wa mapato na
ushiriki wa Watanzania katika umiliki wa kampuni zenye vibali vya uchimbaji
nchini.
Kwa robo nzima ya mwaka, kampuni hiyo inayomilikiwa na
Barrick Gold Corporation kwa asilimia 63.9 imezalisha wakia 191,203 na kuuza
wakia 132,787. Pamoja na takwimu hizo, changamoto za upatikanaji wa vibali na
kupunguzwa kwa uzalishaji kwenye baadhi ya migodi yake kumeathiri kiasi cha
dhahabu iliyopatikana.
Vibali viliathiri uzalishaji wa Mgodi wa North Mara ambao
umetoa wakia 72,011 ndani ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba wakati
Mgodi wa Bulyanhulu ukizalisha wakia 50,094 kutokana na kupunguza operesheni
zake.
“Uzalishaji umezidi matarajio katika Mgodi wa Buzwagi
uliochangiwa na ubora dhahabu iliyopatikana. Tulizalisha wakia 69,097,”
inasomeka taarifa hiyo.
Kuanzia Julai 31, mazungumzo baina ya Serikali na Barrick
yanaendelea kutafuta muafaka wa zuio hilo pamoja na kuongeza faida kwa kila
upande.
Miongoni mwa yanayojadiliwa kwenye mazungumzo hayo ni faini ya Dola 190
bilioni za Marekani (zaidi ya Sh424 trilioni) ambayo Acacia imeandikiwa na
Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwa ni kodi iliyokwepwa pamoja na riba yake.
Tangu kuanza kutekelezwa kwa zuio hilo, bei ya hisa za
kampuni hiyo iliyoorodheshwa Soko la Hisa London (LSE) na Dar es Salaam (DSE)
imeshuka kutoka Sh12,000 mpaka Sh5,000 kila moja.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment