Akizungumza na vyombo vya habari, waziri wa fedha wa Tanzania Mhe. Saada Salum Mkuya alisema”, sisi kama nchi tuliwasilisha nini tunaona katika utekelezaji wa mipango ya Benki. Tumeshukuru sana Benki ya Dunia kwa kuendeleza mipango ya kuweza kusaidia nchi za kiafrika, hususan kwenye mipango ya kujenga miundo mbinu ya kiuchumi kama vile barabara, kilimo pamoja na miundo mbinu ya maji na umeme”.
“Lakini vilevile tumeonyesha wasiwasi wetu kutokana na sera ambazo Benki ya Dunia imeziweka, kama vile kuangalia sera zile za watu wa kiasili ya kiafrika, sisi tumehisi mbali ya nia nzuri na njema ya Benki hii ya Dunia, lakini inaweza kuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi zetu kwa sababu sera hiyo inaweza kutumika kuigawa nchi ambayo misingi yake imekuwa ikijengwa kwa umoja kutoka uhuru”. Alisistiza Mkuya.
Hakuishia hapo aliendelea kutoa mfano kuwa “sisi watanzania tumekuwa wamoja ingawa tuna lugha mbalimbali kutokana na makabila tofauti. Lakini tumekuwa pamoja kwa kipindi cha miaka 50. Kwa hiyo tumeona sera hiyo isije ikatumika kwa ajili ya kuwa kigezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini. Sisi kama wa Afrika na viongozi wa Afrika tunashirikiana kuona kuwa sera zinazowekwa hazitukwamishi”.
Hali hii ya kudai uasilia (indigenous) imeibuka zaidi katika miongo hii miwili, wakati kukiwa kumejitokeza watu wanaodai kuwa wao hawatambuliki na hoja hii inaihusu hasa nchi ya Tanzania.
Mawaziri wa Fedha kutoka Afrika wamejadili mambo mbali mbali ambapo ni pamoja na masuala ya maendeleo na mahusiano yao na Benki ya Dunia. Katika Mkutano huo wa kisheria Mkurugenzi Mtendaji ndiye ambaye amewasilisha maazimio ya Benki katika kipindi cha miezi sita. Aliongeza Mkuya.
Aidha katika mkutano huo pia walizungimzia suala la Ebola. “Kwa kweli wamekubali kusaidia nchi zile ambazo zimekumbwa na gonjwa hili lakini wamezitaka nchi za afrika na zenyewe kushirikiana katika kupambana na gonjwa hili”. Alimalizia Mkuya.
Mikutano hiyo bado inaendelea hapa mjini Washington DC. Hali ya hewa ni baridi kiasi.
Imetolewa na Msemaji: Wizara ya Fedha
Ingiahedi C. Mduma
Washington DC
18/04/2015
No comments:
Post a Comment