Katika makubaliano hayo, kiasi cha fedha zipatazo Dola za Kimarekani 950,000 zitatolewa kwa ajili ya Mradi wa Dirisha la Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Window) ambazo zitachangiwa kwa pamoja kati ya ICF na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kurahisisha taratibu na kufanya huduma zote zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji kupatikana haraka, kwa ufanisi, na bila kupoteza muda na gharama kwa wawekezaji. Gharama hizo za Dola za Kimarekani 950,000 zitachangiwa kwa ICF kutoa Dola za Kimarekani 650,000 na Serikali ya Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) itachangia Dola za Kimarekani 300,000.
Chini ya makubaliano haya, ICF itakisaidia Kituo cha Uwekezaji (TIC) kukuza, kuinua na kulitangaza Dirisha la Uwekezaji na kuimarisha uwezo wake katika kuwezesha na kufuatilia uwekezaji nchini Tanzania. Ikumbukwe kwamba mnamo mwaka 2014 TIC ilianzisha huduma ya kimtandao ya Dirisha la Uwekezaji ambapo huduma mbalimbali zinazohusu uwekezaji zinapatikana kwa pamoja. Chini ya utaratibu huu wawekezaji wa ndani na wa nje wanaweza kutuma maombi ya huduma wanazohitaji kabla ya kufanya biashara Tanzania.
Hivyo basi, chini ya Mradi huu ambao Makubaliano yake yamesainiwa jana, Dirisha la Uwekezaji kupitia juhudi za kimawasiliano na kuimarisha uwezo wa utendaji kazi wa Kituo cha Uwekezaji zitafanyika. Mpango huu utasaidia kuzileta huduma zote zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji karibu zaidi na wananchi kupitia dirisha la moja (One Stop Shop) kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kama vile TRA, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, SSRA (Mamlaka ya Hifadhi za Jamii) na BRELA kwa kutumia mfumo wa kielectronikia ili kuleta ufanisi zaidi. Kwa sasa Kituo cha Uwekezaji kinao Maafisa Waandamizi kutoka TRA, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Viwanda na Biashara, BRELA, na Wizara ya Ardhi hivyo kwa kutumia Dirisha hili la Uwekezaji, maafisa hawa wataweza kutoa huduma zilizo bora na za kisasa, bila kuchelewa na kwa ufanisi mkubwa.
Matarajio ya Mradi huu ni kuimarisha mtazamo chanya kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwa Tanzania ni sehemu iliyo bora kabisa kuwekeza na hii itasaidia kuongeza uwekezaji mwingi nchini na kutengeneza ajira nyingi zaidi kwa watanzania.
Akizungumza wakati wa kutiwa saini Makubaliano hayo kati ya ICF na TIC, Mwenyekiti mwenza wa ICF Benjamin Mkapa alisema, “ICF ina furaha kubwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini katika kukuza na kuimarisha huduma wanazohitaji wawekezaji. Biashara zote hususan zilizo ndogo zinahitaji kuwa na mazingira yaliyo mazuri watakayofanyia shughuli zao. Kwa kuwa na Dirisha la Uwekezaji, biashara nyingi zitaweza kukua, kuongezeka na kushamiri kwa haraka. Wafanyabiashara na wawekezaji hawa wataweza pia kuchangia sana katika kuzalisha ajira na hatimaye kuboresha kipato kwa watanzania hapa nchini”
Aidha, kwa upande wa Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji Mheshimiwa Christopher Chiza alisema, “Mara Mradi huu wa Dirisha la Uwekezaji Tanzania utakapokamilika, utasaidia kuboresha mazingira ya biashara na ushindani nchini. Kwa muda wa miaka michache iliyopita nafasi ya Tanzania kimataifa katika kufanya biashara kwa mujibu wa ripoti mbalimbali imekuwa hairidhishi, ishara ambayo sio nzuri kwa wawekezaji na sekta binafsi. Kukamilika kwa mpango huu ambao utawezesha usajili mbalimbali wa biashara kufanyika kwa njia ya kielekroniki utafanya taratibu za biashara kuwa rahisi kabisa kwa kuondoa vikwazo na urasimu katika uwekezaji.
No comments:
Post a Comment