Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Friday, 28 November 2025

STANBIC YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA MILIONI 19 KWA HOSPITALI ZA MWANZA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana (katikati), akipokea vitanda 10 na magodoro yake, mashuka 200 na viti vya magurudumu 10 kutoka kwa Meneja wa Benki ya Stanbic Tawi la Mwanza, Geofrey Makondo. Kushoto ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kwandu Mashuda, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Egidy Teulas, na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Zena Kapama (kulia), wakishuhudia.

Mwanza, Novemba 27, 2025 — Benki ya Stanbic Tanzania imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 19 kwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya Hospitali za Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. Vifaa hivyo vinajumuisha vitanda, mashuka na viti mwendo (wheelchairs) kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya katika mkoa huo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Meneja wa Benki ya Stanbic Tawi la Mwanza, Geofrey Makondo, alisema benki hiyo imekuwa na utaratibu endelevu wa kurudisha faida kwa jamii kupitia programu zake za uwajibikaji wa kijamii (CSR).

“Kama wadau wa maendeleo ya sekta ya afya, tumelazimika kutoa msaada huu ili kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali kuboresha huduma za afya. Mpango huu ni sehemu ya uwajibikaji wetu kwa jamii, sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya Stanbic kutoa huduma nchini Tanzania,” alisema Makondo.

Makondo aliongeza kuwa sekta ya afya ina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii na kwamba msaada huo unalenga kuongeza ufanisi wa watoa huduma sambamba na kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Kwa upande wa serikali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Erikana Balandya, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alishukuru Benki ya Stanbic kwa mchango huo muhimu akisema utasaidia kuongeza chachu kwenye utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Naye Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Mwanza, Dkt. Kwandu Mashuda, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, Jesca Lebba, alieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha miundombinu ya vituo vya afya, huku akiishukuru benki kwa kuendelea kuwa mshirika wa karibu katika afya ya jamii.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Zena Kapama, aliwataka wadau wengine kujitokeza na kuunga mkono jitihada za kuboresha huduma za afya katika mkoa huo.

Hatua hii ya Benki ya Stanbic inaendeleza rekodi yake ya kuwekeza kwenye miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania, ikilenga kukuza ustawi wa jamii na kuunga mkono maendeleo endelevu.



No comments:

Post a Comment