ARUSHA, OKTOBA 6, 2025 — Benki ya NMB imezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja (CSW) 2025, huku ikiahidi kuboresha zaidi huduma zake na kusisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa kinara wa huduma bunifu, jumuishi, na zinazokidhi mahitaji halisi ya soko.
Viongozi wa benki hiyo wamesema kaulimbiu ya mwaka huu, “LENGO LINAWEZEKANA (MISSION: POSSIBLE),” si maneno tu, bali ni ahadi wanayoitekeleza kila siku kama sehemu ya utamaduni wa kuyapa maslahi ya wateja kipaumbele.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Arusha, Afisa Mkuu wa Huduma Shirikishi, Bi. Nenyuata Mejooli, aliyemuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema kaulimbiu hiyo inaakisi mwelekeo mpya wa benki katika kuimarisha huduma bora kwa wateja wake.
“Kaulimbiu ya mwaka huu inaonesha kwamba huduma bora si ndoto tu, bali ni dhamira tunayotekeleza kila siku kwa kuwapa wateja wetu thamani halisi,”
alisema Bi. Mejooli katika hafla hiyo iliyoambatana na burudani na wimbo maalum wa kuwaenzi wateja waaminifu wa benki hiyo.
Aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamejikita katika juhudi endelevu za kuboresha huduma kwa njia jumuishi — zikiwemo teknolojia bunifu na uwekezaji katika rasilimali watu.
“Kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya NMB inatambua na kuthamini imani kubwa mliyonayo kwetu. Hili linatuchochea kuendelea kuboresha, kuwekeza na kubuni huduma bora zaidi kwa ajili yenu,” alisisitiza Bi. Mejooli.
Wakati wa maadhimisho ya mwaka jana, NMB ilizindua kampeni kubwa ya huduma chini ya kaulimbiu “SISI NI HUDUMA – TUMEKUPATA!”, iliyolenga kuboresha huduma za kibenki kulingana na mahitaji halisi ya wateja.
Bi. Mejooli alisema miongoni mwa mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo ni kuboresha huduma ya JIRANI, msaidizi wa kidijitali wa NMB anayeendeshwa kwa akili bandia (AI), ambaye sasa ana uwezo wa kuwasaidia wateja kununua bima moja kwa moja kupitia simu zao.
Aidha, NMB imeboresha huduma ya NMB MKONONI, ambayo sasa inaruhusu kununua na kuuza hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), pamoja na uhamisho wa fedha hadi TZS milioni 30 kwa siku.
Huduma hiyo pia inatoa mikopo ya papo kwa papo (Mshiko Fasta) yenye muda wa marejesho hadi miezi mitatu, malipo ya bili kwa urahisi, na utengenezaji wa kadi za kidijitali kwa ajili ya manunuzi mtandaoni.
Ili kuongeza ufanisi, benki pia imeanzisha mifumo ya kudhibiti foleni katika baadhi ya matawi, na kuongeza usambazaji wa mashine za kuweka fedha (CDMs) nchi nzima, hatua inayolenga kuwapa wateja uwezo zaidi wa kujihudumia.
“Pamoja na kuwekeza katika teknolojia, bado watu wetu ni kiini cha maboresho ya huduma tunazozitoa kwa ufanisi mkubwa,”
alibainisha Bi. Mejooli, akisisitiza kuwa nguvu kazi ya NMB ndiyo mhimili wa utoaji bora wa huduma.
Kupitia uwekezaji wa kimkakati katika huduma na uaminifu wa kudumu kutoka kwa wateja wake, NMB imeendelea kuwa benki kubwa na bora zaidi nchini Tanzania kwa vigezo vya mtaji wa soko, ubunifu wa kifedha, na mchango wake katika pato la taifa.
Akihitimisha hotuba yake, Bi. Mejooli aliwaalika wateja kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za Wiki ya Huduma kwa Wateja, kutoa maoni, na kujifunza zaidi kuhusu mwelekeo mpya wa huduma za benki hiyo.
Kwa upande wao, wateja kupitia mwakilishi wao Bi. Juliana Olutu, waliipongeza benki kwa kuendelea kutanguliza maslahi ya wateja katika shughuli zake na kuisihi iendelee kuwekeza katika maboresho ya huduma.
Naye Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw. Filbert Mponzi, alisisitiza kuwa kuwahudumia wateja kwa ubora, uharaka, na ufanisi ni jukumu la msingi la benki hiyo.
“NMB itaendelea kujizatiti kuboresha huduma zake kwa kuzingatia mahitaji ya wateja ili kuhakikisha wanapata huduma bora, za haraka, na zenye ufanisi zaidi,”
alifafanua Bw. Mponzi.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment