Benki ya Equity imeandaa kongamano maalum kwa ajili ya wafanyabiashara na wajasiriamali nchini, chenye lengo la kuwajengea uwezo wa kukuza biashara na kupata fursa za kifedha kupitia mikopo.
Kongamano hilo limekusanya wadau mbalimbali kutoka sekta ya biashara na fedha kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wengi, hususan tatizo la kutopata mikopo kutokana na kukosa utambulisho wa kifedha.
Akizungumza katika kongamano hilo, Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub, alisema changamoto kubwa kwa wajasiriamali ni kutokutambulika katika mifumo ya benki.
“Wajasiriamali wengi hawajengi historia ya kifedha kwa sababu fedha zao haziendi kupitia benki. Hali hii inasababisha wakose rekodi ya kuonyesha mwenendo wa biashara zao. Equity imejipanga kusaidia kundi hili kwa elimu ya kifedha na mifumo rahisi ya kibenki ili kuwawezesha kukidhi vigezo vya kupata mikopo,” alisema.
Kwa upande wake, Emerald Mutajwaa, Meneja Biashara wa Benki ya Equity Mkoa wa Mwanza, alieleza kuwa benki imekuwa ikijikita katika kusogeza huduma karibu na wateja wake ili kuhakikisha hata wajasiriamali wa mikoani wanapata nafasi ya kufaidika na mikopo.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mfanyabiashara, awe mdogo au mkubwa, anapata nafasi ya kutumia huduma za kibenki ili kuboresha biashara yake,” alisisitiza.
Akichangia mjadala, Kechu Nkya, mmoja wa wafanyabiashara waliopata mwaliko, alibainisha umuhimu wa elimu ya namna ya kujenga historia ya kifedha.
“Changamoto kubwa siyo tu ukosefu wa mtaji, bali pia kutokuelewa taratibu za kibenki. Kongamano hili limenipa mwanga mpya kuhusu umuhimu wa kutumia benki katika kila hatua ya biashara ili kujiwekea sifa ya kupata mkopo kwa urahisi,” alisema.
Kwa kuandaa kongamano hilo, Benki ya Equity imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwa mshirika wa karibu wa wafanyabiashara nchini, ikilenga kuwainua wajasiriamali kupitia upatikanaji rahisi wa elimu ya kifedha na huduma za mikopo.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment