Dar es Salaam, 16 Desemba 2025 – Taasisi ya harakati za kijamii ya Hadithi Nzuri, kwa kushirikiana na kampuni ya WeMedia, imetekeleza tukio la kijamii la WE GIVE BACK 2025, mpango mahsusi wa kurejesha matumaini, hadhi, na fursa kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi jijini Dar es Salaam.
Mpango huu unakuja wakati ambapo changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na uhamiaji wa mijini inaendelea kuongezeka kwa kasi katika miji mikubwa ya Tanzania. Kupitia WE GIVE BACK 2025, Hadithi Nzuri imeonesha kwa vitendo hali halisi ya kutengwa inayowakumba vijana wanaoishi mitaani, huku ikibainisha kwa uwazi uwezo mkubwa waliyonayo endapo watapatiwa fursa sahihi na kuondolewa vikwazo vya kimfumo.
Vijana 156 Washiriki, Changamoto Zikibainishwa kwa Undani
Tukio la WE GIVE BACK 2025 liliwahusisha watoto na vijana 156 kutoka maeneo ya Kijitonyama – Sayansi, Ubungo, Coco Beach, Kinondoni – Morocco, na Kariakoo. Kwa mujibu wa takwimu za mpango huo, washiriki wengi wameishi mitaani kwa kipindi kinachokadiriwa kati ya miezi mitatu hadi miaka 15.
Ripoti ya WE GIVE BACK 2025 inaonesha kundi la vijana wenye umri mdogo, ari ya kujifunza, na dhamira ya kujenga upya maisha yao. Hata hivyo, juhudi zao zinakwazwa na changamoto za kimfumo zikiwemo:
- Ukosefu wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
- Makazi yasiyo na uhakika
- Upatikanaji mdogo wa mafunzo ya ujuzi
- Changamoto za afya na msaada wa kisaikolojia
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni washiriki wanne tu kati ya 156 waliokuwa na vitambulisho vya NIDA, huku vijana 86wakihitaji kwa dharura kusajiliwa – hali inayozuia kabisa upatikanaji wa ajira, mafunzo, na ujumuishwaji rasmi katika jamii.
Hamasa Kubwa kwa Mafunzo ya Ufundi
Pamoja na changamoto hizo, ripoti inaonesha hamasa kubwa ya vijana kushiriki mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, hususan katika fani za:
- Udereva na ufundi wa magari
- TEHAMA
- Ukarimu na hoteli (hospitality)
- Uchomeleaji (welding)
- Umeme
Hali hii inaonesha wazi kuwa vijana hawa hawakosi nia ya kujibadilisha, bali wanakosa mifumo wezeshi ya kuwavusha kutoka mazingira hatarishi kwenda maisha yenye staha.
“Hatuna Kizazi Kilichopotea” – Hadithi Nzuri
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bw. Baraka Peneza, Mwanzilishi wa Hadithi Nzuri, alisema kazi ya taasisi hiyo huanza kwa kusikiliza kwa makini.
“Kwa kushiriki chakula pamoja, tunaunda maeneo salama yanayowawezesha vijana kueleza wao ni nani, wanafahamu nini, na wana matumaini gani. Tunachoona si kizazi kilichopotea, bali ni vijana wanaohitaji fursa, mwongozo, na mtu wa kuambatana nao katika safari ya maisha,” alisema Bw. Peneza.
Mbinu ya Hadithi Nzuri inaunganisha usimulizi wa hadithi na vitendo, ikitumia chakula kama daraja la kujenga imani na kubaini mahitaji halisi ya vijana. Zaidi ya misaada ya haraka kama chakula, mavazi, viatu, blanketi, na mahitaji ya usafi, mpango huu unaweka mkazo kwenye suluhu za muda mrefu ikiwemo:
- Upatikanaji wa nyaraka za utambulisho
- Mafunzo ya ufundi stadi
- Njia za ajira
- Rufaa za huduma za afya
- Mwongozo wa kihisia na kisaikolojia
WeMedia Yaimarisha Usimulizi wa Hadithi za Mabadiliko
Ushirikiano na WeMedia uliimarisha uwezo wa mpango huu katika kurekodi manufaa na kutoa jukwaa kwa sauti ambazo mara nyingi hazisikiki.
WeMedia ilieleza kuwa ushirikiano huo unaendana na dhamira ya kampuni hiyo ya kusaidia chapa na mashirika kusimulia hadithi zenye kuleta mabadiliko chanya. Kupitia WE GIVE BACK 2025, kampuni hiyo iliona fursa ya kusaidia kusimulia hadithi za watoto na vijana wanaoishi pembezoni mwa jamii – kuhakikisha wanaonekana, wanaeleweka, na wanapewa nafasi ya haki katika maendeleo ya jamii.
Wito wa Ushirikiano kwa Suluhu Endelevu
Washirika wa tukio hilo akiwemo Dough Works (KFC & Pizza Hut), Chemicotex (Tressa & Whitedent), GSM Beverages, Demichtoph, Tembomax, Ruby International, Keds Limited, Men-Men-Men the Podcast, na Code Studios, wamesisitiza kuwa maarifa yaliyopatikana yanaonesha hitaji la suluhu za muda mrefu zinazoongozwa na jamii husika, badala ya misaada ya muda mfupi.
Hadithi Nzuri imetoa wito kwa:
- Taasisi za serikali
- Vyuo vya ufundi stadi
- Waajiri
- Asasi za kiraia
- Viongozi wa jamii
kushirikiana kuondoa vikwazo vya kimfumo, hususan vinavyohusiana na upatikanaji wa vitambulisho, mafunzo ya ujuzi, na njia zenye hadhi za kuingia kwenye ajira na maisha ya kijamii.
Mustakabali Wenye Matumaini kwa Wote
Dira ya Hadithi Nzuri inabaki kuwa ni kuona Tanzania yenye matumaini kwa kila mtu, ambapo jamii zinaungana kusaidiana, kujenga heshima, na kuandaa mazingira rafiki kwa maendeleo endelevu ya vijana kabla ya kutegemea msaada wa nje.
Kuhusu Hadithi Nzuri
Hadithi Nzuri ni taasisi ya harakati inayoongozwa na jamii nchini Tanzania, inayotumia usimulizi wa hadithi, kushiriki chakula, na kujenga imani ili kuwaunga mkono watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi. Kazi yake inalenga heshima, ujumuishaji wa kijamii, na suluhu zinazoongozwa na jamii husika, zinazokidhi mahitaji ya haraka na kuweka msingi wa fursa za muda mrefu.
No comments:
Post a Comment