Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Monday, 15 December 2025

ATE YAKUTANA NA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU – KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), tarehe 13 Desemba 2025, kimekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu (Mb), katika Mkutano wa 72 wa Bodi ya Uongozi wa ATE uliofanyika katika Hoteli ya Seacliff, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe wa Bodi ya Uongozi wa ATE wanaowakilisha sekta mbalimbali za uchumi, wakiwemo Bi. Caroline Mugalla, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), pamoja na wanachama wa ATE kutoka taasisi na makampuni mbalimbali ikiwemo NMB Bank, Chemi Cotex, ALAF, TSIA na Heritage Insurance.

Waajiri ni Injini ya Uchumi

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Sangu alitoa ufafanuzi kuhusu dhana ya Mahusiano ndani ya Wizara yake, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Waajiri na Wafanyakazi katika kujenga mazingira bora ya kazi. Alibainisha kuwa Waajiri ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa kwa kuwa wanazalisha ajira, hulipa kodi, huwekeza katika shughuli za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa maendeleo ya nchi.

Aidha, Mheshimiwa Waziri alieleza maeneo muhimu yanayohitaji maboresho katika sekta ya kazi na ajira, huku akiahidi kushirikiana kwa karibu na Waajiri kuyafanyia kazi kwa pamoja. Pamoja na hilo, aliwakumbusha Waajiri kuendelea kuzingatia Sheria za Kazi na kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi.

Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa ATE 2026–2030

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Sangu alizindua rasmi Mpango Mkakati wa ATE wa mwaka 2026 hadi 2030, na kuipongeza ATE kwa kuandaa mkakati unaoendana na vipaumbele vya Taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dhamira ya ATE kwa Waajiri

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Bw. Oscar Mgaya, alisisitiza dhamira ya Chama hicho kuendelea kusimamia na kutetea maslahi ya Waajiri nchini. Alieleza kuwa ATE itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuimarisha sekta ya ajira na kazi, kwa lengo la kuongeza tija, ushindani na ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Mkutano huo umeonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Waajiri, kama msingi muhimu wa kujenga mazingira bora ya kazi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini.




No comments:

Post a Comment