Benki ya NMB kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Biashara, imewatambua wanafunzi kumi bora katika kozi kumi waliomaliza masomo mwaka huu kwa hafla maalum ya utoaji zawadi, ikiwatambua kwa mafanikio yao ya kitaaluma na juhudi kubwa iliyowaletea ufaulu.
Hafla hiyo, iliyofanyika siku moja kabla ya kuanza kwa mahafali ya chuo hicho, ilihusisha utoaji wa zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslimu, vyeti, na fursa za mafunzo kazini kwa washindi hao. Wawakilishi wa Benki ya NMB walipongeza juhudi za wahitimu na chuo kwa ujumla katika kukuza vipaji na maendeleo ya kitaalamu.
Kwa niaba ya Benki ya NMB, Mgeni Rasmi wa hafla hiyo na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Kituo cha Utaalamu wa Benki ya NMB, Joanitha Mrengo, alielezea fahari ya benki katika kuunga mkono juhudi za vijana, hususani za kitaaluma.
“Kwetu sisi ni fahari kubwa kushiriki katika kutambua bidii na juhudi za vijana hawa wadogo. Leo tunashuhudia nidhamu, uvumilivu na ubora wao wa kitaaluma ukileta majibu stahiki. Benki ya NMB itatengeneza fursa kuanzia za ajira na hata za mafunzo kazini ambazo tunaamini zitawawezesha wataalamu hawa kustawi katika soko la ajira,” alisema Mrengo.
Mrengo pia aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Benki ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaendelea kuwa wa dhati, ukiwapa wanafunzi nafasi za kujifunza wakiwa masomoni, hivyo kuchangia katika kuzalisha wataalamu bora zaidi katika sekta ya kifedha.
“Mbali na mafunzo wakiwa kazini, tumekuwa na ushirikiano wa karibu na Chuo kikuu katika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, pamoja na makubaliano makubwa ya kushirikiana katika masuala ya kitehama,” alibainisha.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu, akisema:
“Ushirikiano wetu na Benki ya NMB unaboresha ubora wa elimu tunayoitoa na unachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa. Pamoja, tunatengeneza viongozi watakaochochea maendeleo ya Tanzania.”
Aidha, Profesa Boniface alibainisha kuwa Chuo kikuu kitaendelea kutumia wataalamu mbalimbali, ikiwemo wale wa NMB, kutoa mihadhara maalum kwa wanafunzi, ili kuwapa maarifa ya vitendo katika nyanja zao na kuwaandaa vyema kwa changamoto za baadaye.
Mkuu wa Idara ya Wanafunzi wa Chuo, Profesa Omary Mbura, alielezea nafasi ya NMB kama mshirika wa kina:
“Benki ya NMB imekuwa ikituunga mkono si tu kwa msaada wa kifedha bali pia kwa kushiriki kikamilifu katika miradi yetu ya kitaaluma na jamii.”
Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio, alisema hafla hiyo ni hatua ya kimkakati kuelekea kuimarisha ushirikiano unaowanufaisha wanafunzi, wafanyakazi wa chuo, na uchumi wa taifa:
“Tunatarajia kuimarisha zaidi uhusiano huu, ambao unachangia katika maendeleo ya uchumi wetu na pamoja, tunajenga mustakabali mzuri wa Tanzania.”
Ushirikiano huu unaonyesha dhamira ya pamoja ya ubora, ubunifu, na ukuaji wa kitaaluma, huku Benki ya NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakijenga msingi imara wa kuendeleza vipaji na kuwajenga viongozi wa kesho.
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)


No comments:
Post a Comment