Benki ya Equity Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kukuza ujasiriamali nchini kwa kuwawezesha wahitimu wa Anna Collection Fashion Academy (AFA) kupitia elimu ya fedha, mitaji, mafunzo ya usimamizi wa biashara na fursa za maonesho ya ubunifu (exposure). Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa ujuzi wanaoupata vijana hao unawageuza kuwa wajasiriamali wenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika mahafali ya nne ya AFA, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Tanzania, Isabella Maganga, alisema benki hiyo imejipanga kuwaunga mkono zaidi ya wahitimu 350 kupitia programu maalumu za kuwajengea uwezo katika masuala ya biashara, ujasiriamali, usimamizi wa fedha na matumizi sahihi ya mikopo.
“Wahitimu wanapaswa kuwa na nidhamu, bidii, kuheshimu muda wa wateja na kubadilisha ubunifu wao kuwa biashara halisi zinazowawezesha kiuchumi,” alisema Maganga, akibainisha kuwa kupitia kitengo cha Huduma kwa Wanawake na Vijana, benki hiyo inatoa mafunzo na mikopo nafuu kwa wanafunzi wanaotaka kuanzisha na kuendeleza biashara.
Maganga aliongeza kuwa sekta ya ushonaji na ubunifu wa mavazi inastahili kupewa heshima na uangalizi kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwa vijana wengi. Aliitaja sekta hiyo kuwa injini muhimu ya uchumi, inayowawezesha vijana kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Anna Collection Fashion Academy, Anna Peter, aliwataka wahitimu kuthamini ubunifu wao na kuutumia kama ajira yenye thamani, inayohitaji nidhamu, ubora, uwezo wa kutatua matatizo ya wateja na utoaji wa bidhaa kwa bei inayoendana na thamani halisi.
“Wahitimu wa AFA si wabunifu tu; ni wakombozi wa uchumi wa nchi,” alisema Anna, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya AFA na Equity Bank utaendelea kujenga kizazi kipya cha wabunifu watakaochangia kwa kiwango kikubwa uchumi kupitia ubunifu, usimamizi wa fedha, na ukuaji wa tasnia ya mavazi nchini.
Mpango huo wa pamoja unatarajiwa kuimarisha uwezo wa vijana kuingia sokoni wakiwa na ujuzi, maarifa na mtaji unaohitajika ili kuendeleza biashara endelevu, hivyo kuongeza wigo wa ajira na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
No comments:
Post a Comment