Dar es Salaam, 29 Septemba 2025 – Vodacom Tanzania kupitia asasi yake ya kijamii imeingia makubaliano ya ushirikiano na Heart Team Africa Foundation, taasisi inayofanya kazi chini ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), katika juhudi za kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini. Hafla ya utiaji saini imefanyika sambamba na Siku ya Moyo Duniani 2025, chini ya kaulimbiu “Don’t Miss a Beat”, ikisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua mapema na kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa afya ya moyo.
Changamoto za Maradhi ya Moyo kwa Watoto
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili:
- Watoto 2 kati ya kila 100 huzaliwa na ugonjwa wa moyo (Congenital Heart Disease – CHD).
- Asilimia 3 ya watoto wenye umri wa miaka 5–15 huathirika na Ugonjwa wa Moyo wa Rheumatic (RHD), hali inayoweza kuzuilika kwa matibabu ya mapema ya maambukizi ya koo.
- Zaidi ya watoto 4,000 huhitaji upasuaji kila mwaka, huku JKCI ikikabiliwa na orodha ya zaidi ya watoto 350 wanaosubiri huduma hiyo.
Serikali hufadhili takribani asilimia 70 ya gharama za matibabu, lakini familia nyingi hupata changamoto kubwa kufanikisha asilimia 30 inayobaki.
Kauli za Viongozi
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alisema:
“Kila takwimu inawakilisha mtoto mwenye ndoto na mzazi mwenye matumaini. Ushirikiano huu utatusaidia kupunguza pengo kati ya uhitaji na upatikanaji wa huduma, ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanaishi maisha yenye afya njema.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Heart Team Africa Foundation, Dkt. Naizihijwa Majani, aliongeza:
“Kila siku tunaona jinsi gharama za matibabu zinavyoweza kuwa kizuizi kati ya mtoto na mustakabali wake. Ushirikiano huu sio tu msaada wa kifedha, bali ni njia ya kuokoa maisha. Kwa pamoja, tunajenga Tanzania ambayo hakuna mzazi anayelazimika kuchagua kati ya umasikini na mapigo ya moyo ya mtoto wake.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisema:
“Huu ni wakati wa kuchukua hatua na ndiyo maana tuko hapa. Makubaliano haya ni ishara thabiti ya kugeuza imani kuwa vitendo kupitia Mpango wa Amini. Tukishirikiana na JKCI, tunafungua kesho ambayo hakuna mtoto atakayepoteza maisha kwa kukosa huduma zinazoweza kuokoa maisha.”
Historia ya Mpango wa Amini
Mapema mwaka huu, Vodacom Tanzania Foundation ilizindua Amini Initiative Visiwani Zanzibar, ikiahidi kudhamini watoto 150 kwa kugharamia asilimia 30 ya gharama za matibabu. Mpaka sasa watoto 38 wenye umri kati ya miezi miwili na miaka 14 wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio.
Wito kwa Wadau
Vodacom Tanzania Foundation, JKCI na Heart Team Africa Foundation wametoa wito kwa serikali, kampuni binafsi na wadau mbalimbali kushirikiana nao katika jukumu hili la kuokoa maisha ya watoto:
“Huu ni wito wa kitaifa. Tunawaalika serikali, kampuni na watu binafsi kusimama nasi, ili mtoto wa Kitanzania asibaki akisubiri upasuaji unaookoa maisha.”


.jpeg)
No comments:
Post a Comment