Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, ameendelea na mikutano yake na wateja jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa ziara zinazolenga kujenga uelewa na kuimarisha huduma za benki baada ya kukamilika kwa maboresho makubwa ya mfumo mkuu wa utoaji huduma (Core Banking System).
Akiwa katika tawi la CRDB TPA lililopo katika Jengo la Bandari, Nsekela alikutana na mameneja wa matawi ya Kanda ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na wanahabari. Pia alipata nafasi ya kuzungumza na wateja waliokuwa wakihudumiwa, ambapo aliwashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao wakati wa mabadiliko ya mfumo.
“Kuanzia tarehe 8 Septemba tulihamia kwenye mfumo mkuu wa utoaji huduma za benki ambapo, kwa ukubwa wa mabadiliko yaliyofanyika, baadhi ya wateja wetu walipata changamoto katika akaunti zao na baadhi ya miamala kutofanikiwa. Juhudi za wataalamu wetu zimefanyika usiku na mchana, na hadi jana akaunti zilizokuwa na changamoto zilirudi katika hali yake ya kawaida. Aidha, wateja ambao miamala yao ilikwama walirudishiwa fedha katika akaunti zao na miamala kuendelea kufanyika kwa ufanisi,” alisema Nsekela.
Nsekela alibainisha kuwa uwekezaji katika mfumo huu mpya umezingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wateja. Maboresho hayo yametekelezwa pia katika nchi ambako CRDB inafanya biashara — Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) — na huduma zinaendelea vizuri.
Aidha, mageuzi hayo yanatoa msingi wa Benki kujitanua zaidi kimataifa, hususan baada ya kupata leseni ya kuanzisha ofisi Dubai.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa biashara, Nsekela alisisitiza kuwa licha ya kipindi cha mabadiliko, benki imeendelea kufanya vizuri, jambo linalothibitisha imani ya wateja kwa CRDB. Vilevile aliwashukuru wafanyakazi kwa kujitoa kwao na kuwataka kuendeleza weledi katika kusimamia mfumo mpya ili kuhakikisha unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment