Dar es Salaam, 7 Septemba 2025 – Columbia Africa Healthcare Limited imetangaza rasmi ununuzi wa asilimia 100 wa IST Clinic, moja ya vituo maarufu vya huduma za afya jijini Dar es Salaam. Kupitia hatua hii, kampuni hiyo inaongeza Tanzania kwenye mtandao wake wa vituo vya tiba, sambamba na Nairobi, Kenya.
Ununuzi huu ni sehemu ya mkakati wa Columbia Africa wa kupanua huduma bora, nafuu na zinazomlenga mgonjwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Baada ya mchakato wa muunganiko, IST Clinic itaanza kufanya kazi chini ya jina la Columbia Africa.
HUDUMA ZITAKAZOBORESHWA
Muunganiko huu unatarajiwa kuongeza thamani ya huduma kwa wagonjwa kupitia:
- Ubora wa Juu wa Huduma: mifumo ya kitabibu yenye viwango vya kimataifa na kanuni za usalama.
- Upatikanaji Rahisi: wigo mpana wa vipimo na huduma za kibingwa.
- Huduma Kidijitali: mfumo wa kisasa wa usimamizi wa kliniki, unaorahisisha usajili, miadi na usalama wa kumbukumbu.
- Mwendelezo wa Huduma: timu ya sasa ya madaktari wa IST Clinic itaendelea kuhudumia wagonjwa.
- Programu za Afya na Ustawi: huduma za kinga na ushauri wa kimataifa kwa wagonjwa na familia.
KAULI ZA VIONGOZI
Akizungumzia ununuzi huo, Dkt. Sumit Prasad, Mkurugenzi Mtendaji wa Columbia Africa alisema:
“Ununuzi huu si tu hatua ya ukuaji – bali ni ahadi ya kuleta huduma za afya za viwango vya kimataifa karibu na jamii za Tanzania, huku tukidumisha mahusiano ambayo wagonjwa wameyajenga na madaktari wao.”
Ype Smit, MD, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa IST Clinic, aliongeza:
“Kwa zaidi ya miaka 25, IST Clinic imekuwa ikitoa huduma zinazomlenga mgonjwa moja kwa moja jijini Dar es Salaam. Kujiunga na Columbia Africa kunatupa nafasi ya kuchanganya historia hii na teknolojia ya kisasa na viwango vya kimataifa.”
IST CLINIC NA SAFARI YAKE
Tangu kuanzishwa mwaka 1997, IST Clinic imekua mtoa huduma anayeaminika jijini Dar es Salaam, ikitambulika kwa tiba ya kibinafsi, huduma endelevu na mahusiano ya karibu na familia nyingi nchini.
Kwa zaidi ya robo karne, kliniki hii imejijengea sifa ya utoaji wa huduma bora kupitia timu ya madaktari, wauguzi, maabara na wafamasia.
COLUMBIA AFRICA NA UPANUZI WAKE
Columbia Africa ni sehemu ya Columbia Pacific Management Inc., kampuni yenye makao yake Seattle, Marekani, yenye zaidi ya miaka 40 ya uzoefu katika kuendeleza hospitali na vituo vya huduma za afya duniani.
Kupitia uwepo wake Tanzania, Columbia Africa inalenga kuendeleza mifumo endelevu ya afya katika maeneo yenye ukuaji wa haraka, huku ikiimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa jamii za Afrika Mashariki.
Kwa Tanzania, hatua hii ni ishara ya kuongezeka kwa uwekezaji binafsi kwenye sekta ya afya, sekta muhimu kwa uchumi na ustawi wa jamii.





No comments:
Post a Comment