Dar es Salaam, Julai 18, 2025 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ambao ndio waandaaji wa mbio za NBC Dodoma Marathon, leo imeendelea na maandalizi ya kuelekea mbio hizo kwa kukabidhi rasmi jezi na vifaa maalum kwa mmoja wa wadhamini wakuu wa mbio hizo, kampuni ya GSM Group.
Kupitia kampuni tanzu ya GSM Beverages, GSM Group inadhamini huduma ya maji na vinywaji baridi kwa washiriki wa mbio hizo za sita ambazo zinatarajiwa kufanyika tarehe 27 Julai 2025, jijini Dodoma.
Mbali na udhamini wa maji, GSM Foundation—taasisi ya kijamii ya GSM Group—ni mfadhili mkuu wa ajenda tatu muhimu za kijamii zinazoratibiwa na mbio hizi mwaka huu:
- Kuendeleza mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake,
- Kufadhili wakunga hadi kufikia idadi ya wakunga 200,
- Kuanzisha mpango mpya wa kufadhili masomo ya wauguzi 100 watakaotoa huduma kwa watoto wenye changamoto ya usonji (autism).
Ujumbe kutoka NBC uliongozwa na Mkurugenzi wa Fedha, Bw. Rayson Foya, akiambatana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma, Bw. Godwin Semunyu, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bi. Tatiana Massimba.
Walipokelewa katika makao makuu ya GSM Group jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa GSM Group, Bw. Gharib Said Mohamed (GSM), pamoja na viongozi wengine waandamizi akiwemo Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mhandisi Hersi Said, Mkurugenzi Msaidizi, Bi. Chenedzo Mupukuta, na maofisa wengine wa kampuni hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bw. Foya aliishukuru kampuni ya GSM Group kwa kuwa mdau muhimu wa mbio hizo, akisisitiza mchango wao mkubwa katika kufanikisha malengo ya kijamii kupitia mbio hizi.
“Tupo hapa kukabidhi vifaa hivi kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa GSM Group kwenye mafanikio ya NBC Dodoma Marathon. Mbali na kutoa maji na vinywaji kwa washiriki zaidi ya 12,000, GSM kupitia Foundation yao wamechukua jukumu kubwa zaidi katika kufanikisha ajenda zetu tatu kuu zinazogusa afya ya mama na mtoto na changamoto za watoto wenye usonji,” alisema Bw. Foya.
Kwa upande wake, Mhandisi Hersi Said aliipongeza NBC kwa ushirikiano wa muda mrefu na kwa kutumia michezo kama njia ya kuleta maendeleo na kuokoa maisha ya jamii.
“Sisi GSM Group tunajivunia kuwa mshirika rasmi wa NBC kwenye mbio hizi zenye malengo makubwa ya kijamii. Tunaamini kuwa kwa kushirikiana, tunaweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii. Tunaendelea kuwakaribisha washiriki wote na tumejipanga kuhakikisha wanapata huduma bora ya maji na vinywaji baridi,” alisema.
Naye Bi. Tatiana Massimba, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, alithibitisha kuwa tayari kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi. Alisisitiza kuwa usajili bado unaendelea kupitia tovuti rasmi www.events.nbc.co.tz ambapo:
“Usajili kwa mtu mmoja mmoja ni TZS 45,000, huku usajili wa kikundi (watu 30 au zaidi) ukiwa ni TZS 42,000 kwa kila mshiriki. Tunawaalika Watanzania wote kushiriki katika tukio hili lenye lengo la kusaidia maisha na kuchochea maendeleo ya kijamii.”
📌 Endelea kutembelea blogu yetu kwa taarifa zaidi kuhusu NBC Dodoma Marathon 2025, wadhamini wakuu, mafanikio ya kijamii na namna ya kushiriki au kuchangia ajenda za mwaka huu.
No comments:
Post a Comment