Arusha – Julai 10, 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ameipongeza Benki ya NMB kwa ushirikiano wake wa karibu na Serikali katika kufanikisha matukio mbalimbali ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akizungumza jijini Arusha alipotembelea banda la maonyesho la NMB kabla ya kufungua Mkutano wa 14 wa Watunga Sera wa Sekta ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika, unaofanyika katika ukumbi wa AICC, Dkt. Mpango alieleza kufurahishwa kwake na mchango wa benki hiyo kwa taifa.
“Kila ninapoiona NMB ikishiriki katika matukio mbalimbali yanayoandaliwa na Serikali kama mshirika wa karibu, roho yangu inasuuzika kwa sababu najua kazi wanazofanya na uwezo walionao,” alisema Dkt. Mpango.
WITO WA KUWEKEZA ZAIDI VIJIJINI
Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo kuitaka NMB kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya benki vijijini, ili kuhakikisha Watanzania wanaoishi maeneo ya pembezoni wanapata huduma sawa na wale wa mijini.
“Ni muhimu benki kama NMB kuhakikisha kuwa huduma zake zinafika kila kona ya nchi, ili kila Mtanzania apate haki ya kifedha bila kujali eneo analoishi,” alisisitiza.
NMB YATOA ZAIDI YA BILIONI 6.4 KUISAIDIA JAMII
Akiwasilisha taarifa ya huduma za kijamii, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa NMB, Baraka Ladislaus, alisema benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka kwa ajili ya kuisaidia jamii.
“Kwa mwaka huu pekee, tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 6.4 kusaidia sekta ya Afya, Elimu na Mazingira. Lengo letu ni kurejesha faida kwa jamii inayotuzunguka na kushirikiana na serikali kuhudumia wananchi,” alisema Baraka.
NMB YAUNGA MKONO MIFUKO YA JAMII
Baraka aliongeza kuwa NMB inaendesha kampeni maalum ya kuunga mkono kazi za mifuko ya hifadhi ya jamii katika kuimarisha uchumi wa wanachama, kupunguza utegemezi na kuinua maisha ya wazee.
“Tuna bidhaa maalum kama NMB Hekima Plan, inayolenga wastaafu na wale wanaotarajia kustaafu. Kupitia mpango huu, tunatoa elimu ya kifedha ikiwemo uwekezaji na utunzaji wa mafao ili yawasaidie kwa muda mrefu,” alieleza.
Aidha, alitaja pia mpango mwingine uitwao ‘NMB Jiwekee’, ambao unawawezesha wateja kujiwekea akiba kwa utaratibu wa makato ya moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao kwa kipindi wanachochagua.
MJADALA KUHUSU MIFUKO YA JAMII AFRIKA
Awali, akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema mkutano huo unalenga kujadili jinsi mifuko ya jamii barani Afrika inaweza kusaidia katika maendeleo ya miundombinu.
“Mkutano huu unajadili namna bora ya kuchochea uwekezaji katika miundombinu kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii, ili kupunguza utegemezi wa misaada kutoka mataifa tajiri, hasa katika kipindi hiki cha changamoto za kiuchumi na migogoro ya kisiasa duniani,” alisema Waziri Ridhiwani.
Kwa ushirikiano huu wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi kama NMB, Tanzania inaendelea kuweka msingi imara wa maendeleo shirikishi na endelevu, yanayomlenga mwananchi mmoja mmoja – mijini na vijijini.
Tembelea blogu yetu kwa taarifa zaidi kuhusu sekta ya fedha, maendeleo ya uchumi, benki na masoko ya mitaji.
No comments:
Post a Comment