AngloGold Ashanti imeeleza kwa fahari ushirikiano wake na Taasisi ya Thabo Mbeki katika kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo endelevu barani Afrika, kwa malengo ya kufikia Dira ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063, kupitia kaulimbiu ya “Africa We Want – Afrika Tunayoitaka.”
Akizungumza katika ziara ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye aliambatana na zaidi ya watu 50 kutoka Afrika Kusini waliotembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro, Simon Shayo, Makamu wa Rais wa Masuala ya Uendelevu (Afrika) wa AngloGold Ashanti, alisema kuwa kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya safari ya mageuzi ya bara la Afrika.
“AngloGold Ashanti inashirikiana na taasisi ya Thabo Mbeki kwa sababu tunaamini katika maendeleo ya Afrika kupitia sekta ya madini na tunaamini katika majadiliano ya pamoja kati ya viongozi na wananchi wa kawaida.”
Ushiriki wa Sekta Binafsi Katika Mageuzi ya Bara
Shayo alisisitiza kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika mpango huu hauishii katika biashara pekee, bali una lengo la kuweka daraja la majadiliano ya kina kuhusu mustakabali wa Afrika.
“Kupitia uwekezaji wetu, tunagusa maisha ya watu moja kwa moja – hususan vijana na makundi yaliyo pembezoni – tukichangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi mbalimbali.”
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya AngloGold Ashanti, Taasisi ya Thabo Mbeki, na Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA) unaonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha uongozi bora barani Afrika, kwa lengo la kuondoa utegemezi na kuchochea ukuaji wa ndani kwa kutumia rasilimali kama madini.
Mjadala wa 15 wa Siku ya Afrika: Kuinua Sauti za Bara
Katika mjadala wa mwaka huu, viongozi mashuhuri akiwemo Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete walihusika katika majadiliano ya kuangalia changamoto na fursa za maendeleo ya Afrika, pamoja na hatua za kuziondoa kikwazo zilizopo.
Msafara huo pia ulihusisha viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, na maafisa wa Ubalozi wa Afrika Kusini.
Kumbukumbu ya Mashujaa wa Uhuru
Rais Mbeki aliongoza matembezi ya heshima kutembelea makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliopigania uhuru kupitia chama cha ANC chini ya uongozi wa Rais wa zamani Nelson Mandela. Akiwa pale, alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kuungana na kushirikiana kwa dhati ili kujiletea maendeleo na kuwaenzi mashujaa hao.
“Ziara hii ni ishara ya mshikamano na kumbukumbu ya historia ambayo inatufundisha kuhusu maana ya uhuru, mshikamano, na maendeleo ya pamoja,” alisema Thabo Mbeki.
Viongozi Wengine Watoa Maoni
Vusi Maqabela kutoka Thabo Mbeki Foundation alisema kuwa aliguswa sana na ziara hiyo, hasa baada ya kuona makaburi ya mashujaa ambao alikuwa akijifunza historia yao shuleni.
Prof. Anthoni Van Nieuwkerk kutoka UNISA, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa, alieleza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mjadala wa mwaka huu ni kielelezo cha mchango wake katika historia na maendeleo ya Afrika.
“Kitendo cha Mbeki kupanda mti katika eneo la kihistoria hapa Morogoro ni kumbukumbu ambayo itaendelea kuonyesha undugu uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini,” alisema Prof. Nieuwkerk.
Matukio Yaelekea Kilele cha Hotuba ya Siku ya Afrika
Mfululizo wa matukio ya mjadala huu utaendelea hadi Ijumaa, tarehe 23 Mei, ambapo AngloGold Ashanti itandaa meza ya majadiliano ya ngazi ya juu pamoja na Rais Mbeki. Hafla hiyo itafungwa rasmi na Hotuba ya Siku ya Afrika siku ya Jumamosi, tarehe 24 Mei, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment