Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday 18 January 2018

KIPINDI MAALUM CHA RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KUHUSU ELIMU BURE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua dhidi ya viongozi na watendaji ambao shule za msingi na sekondari zilizopo katika maeneo yao zinawatoza wanafunzi michango mbalimbali kinyume na muongozo uliotolewa na Serikali wa utoaji wa elimu bila malipo. 


Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 17 Januari, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Lazaro Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Said Jafo. 

Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatoa Shilingi Bilioni 23.875 kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo lakini inashangaza kuona bado kuna walimu wanaendelea kuwatoza michango ama kuwarudisha nyumbani wanafunzi ambao wanashindwa kutoa michango hiyo. 

“Nawaagiza Mawaziri, sitaki kusikia mwanafunzi anarudishwa nyumbani kwa kushindwa kutoa michango, na fikisheni maagizo haya kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wote wanaohusika, nikisikia tena mahali jambo hili linaendelea hawa niliowateua mimi wataondoka. 

“Haiwezekani tumefuta ada, halafu walimu wanaamua kuanzisha michango tena mikubwa ambayo watu masikini wanashindwa kusomesha watoto wao, na kama wazazi wanataka kuchangia kitu shuleni wapeleke michango yao kwa Mkurugenzi, lakini sitaki kusikia mwanafunzi anapewa sharti la kutoa mchango ndipo apokelewe shule” amesema Mhe. Rais Magufuli. 

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kupata taarifa kuwa zipo baadhi ya shule ambazo wanafunzi wanadaiwa michango mbalimbali tena kwa kiwango kikubwa ikiwemo chakula, maabara, madawati na ziara za kujifunza, hali iliyosababisha wazazi kushindwa kumudu. Waziri Prof. Joyce Lazaro Ndalichako ameagiza walimu na viongozi wa halmashauri kuwarudisha shule mara moja wanafunzi wote waliorudishwa nyumbani kwa kutotoa michango na pia kurejesha mara moja michango iliyokusanywa kinyume na mwongozo wa Serikali. 

Waziri Mhe. Selemani Said Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya shule ambazo zimetoza michango kinyume na mwongozo wa Serikali ifikapo Ijumaa wiki hii (tarehe 19 Januari, 2018) ili hatua zichuliwe dhidi ya walimu na maafisa elimu ambao kwa makusudi wamekiuka mwongozo huo.

Ikulu Mawasiliano

No comments:

Post a Comment